SHARE

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Balozi Omari Yusuph Mzee ameitaka Yanga kujenga utamaduni wa kuuza wachezaji nje ya nchi kwenda kucheza soka ya kulipwa.

Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Saimon Msuva kuitembelea kambini timu hiyo muda mfupi kabla ya Yanga kucheza na USM Alger.

Msuva aliyecheza Yanga msimu uliopita, amegeuka lulu baada ya kujiunga na klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco.

Balozi Mzee alisema soka ni utajiri ambao taifa, klabu na mchezaji wanaweza kunufaika anapokwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Mchezaji unapofanya vizuri leo unajiuza mwenyewe, ninachotaka kuwaambia viongozi wa Yanga ikiwa imetokea mchezaji anatakiwa nje ya nchi mpeni ruhusa msimzuie.

Itasaidia kuendeleza kipaji na kipato chake, itakuwa na faida kwa Taifa lakini pia itasaidia klabu kupata fedha ambazo zitatumika kusaidia uendeshaji wa klabu,” alisema Balozi Mzee.

Balozi huyo alisema Yanga haipaswi kuruhusu kupoteza pointi kizembe na badala yake inapaswa kuhakikisha inaibuka na ushindi katika kila mchezo ili kusonga mbele kwenye mashindano hayo.

“Yanga ni timu kubwa na wazoefu wa mashindano haya, kwa hatua mliyofikia hatuhitaji kusikia masuala ya kutoka sare kinachohitajika ni ushindi ili baadaye yasije kuanza mambo ya kujilaumu,”alisema Balozi Mzee.

Yanga juzi usiku ilianza vibaya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi baada ya kunyukwa mabao 4-0 na USM Alger ya nchini humu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here