SHARE

Mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Mohammed Rashid, amesema yuko tayari kujiunga na Simba au Yanga.

Akizungumza jana, Rashid alisema klabu yenye dau nono baina ya miamba hiyo itapata saini yake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Rashid mwenye mabao tisa ni mmoja wa washambuliaji ambao wamekuwa wakiwindwa muda mrefu na klabu hizo kongwe nchini. Yanga ilikuwa ya kwanza kutuma maombi katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwaka huu lakini juhudi zao ziligonga mwamba baada ya kubanwa na mkataba.

“Mpira ni kazi yangu kwa hiyo klabu yoyote naweza kujiunga nayo ingawa bado nina mkataba na Tanzania Prisons. Binafsi nina heshimu mkataba wangu,” alisema mshambuliaji huyo.

Mchezaji huyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine endapo atabakiza miezi sita kabla ya mkataba wake kumalizika.

Endapo mshambuliaji huyo atatua Yanga anaweza kuongeza makali kwenye kikosi hicho ambacho msimu huu kimekuwa butu kwenye safu ya ushambuliaji.

Kocha wa zamia wa Yanga, George Lwandamina alimtengeneza Obrey Chirwa kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati kwenye kikosi hicho kujaza nafasi za majeruhi wa muda mrefu Donald Ngoma na Amiss Tambwe.

Pia akitua Simba, Rashid atakutana na changamoto ya kuwania namba mbele ya washambuliaji nyota Emmanuel Okwi na John Bocco.

Mchezaji huyo ameweka bayana anapenda kucheza namba tisa ili kukabiliana ana kwa ana na lango la wapinzani. Okwi anaongoza kwa kufunga mabao 20, John Bocco (14) na Marcel Boniventure Majimaji (13).


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here