SHARE

RAIS Vladimir Putin wa Urusi, ameapishwa kwa muhula wa nne kuliongoza taifa hilo kwenye sherehe iliyofanyika ikulu ya Kremlin, jijini Moscow.

Putin alishinda kiti hicho kwa muhula wa nne kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Machi. Rais huyo alipata asilimia 77 ya kura zote zilizopigwa.

Putin amekuwa Rais wa Urusi kwa miaka 18 na alijiuzulu mwaka 2008 kutokana na ukomo wa muhula ila aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na akaendelea kuiongoza nchi hiyo hadi aliporudi tena madarakani kama rais mwaka 2012.

Katika hotuba ya kuapishwa kwake Rais Putin amesema; “Nachukulia kwamba ni jukumu langu na lengo langu la maisha kuifanyia Urusi chochote, sasa na katika siku za usoni… kama rais nitafanya kadri ya uwezo wangu kuongeza nguvu na ustawi wa Urusi.”

Hata hivyo, kiongozi huyo amekaa kimya kuhusiana na suala la kuondoka kwake madarakani licha ya kuwa ni jambo ambalo hawezi kuliepuka kutokana na ukweli kuwa katiba ya Urusi haimruhusu kuwania tena urais, baada ya kwisha kwa muhula wake huu wa nne mwaka 2024.

CHANGAMOTO

Rais Putin amekuwa na wakati mgumu kufufua uchumi wa taifa hilo baada ya serikali yake kuwekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi, kufuatia hatua yake ya kuipokonya Ukraine eneo la Crimea.

Aidha, kuanguka kwa bei za mafuta duniani mwaka 2016 pia kumechangia kulemaa kwa uchumi wa Urusi, ingawa mwenyewe anakanusha suala la kuzorota uchumi wa taifa lake, akisisitiza linazidi kustawi.

“La muhimu zaidi ni kwamba, katika miaka yote hii nchi imekuwa ikistawi… haijapambana tu na matatizo yaliyoibuka bali ilisonga mbele na kuongeza uwezo wake,” anasema.

Hata hivyo, inaripotiwa kwamba kuapishwa kwake hakujawafurahisha wengi, ingawaje watu wake wa karibu wameandaa sherehe ndogo tu ambayo haitajumuisha karamu ya kifahari ya chakula ili umma usiwe na picha mbaya kuhusu serikali yake.

UPINZANI

Upinzani nchini Urusi haujaridhishwa na hatua ya rais huyo kuingia madarakani kwa muhula wa nne kwani kulikuwa na maandamano yaliyosababisha kamatakamata.

Serikali za nchi za Magharibi na wanaharakati wa haki za binadamu wameelezea kughadhabishwa na hatua hiyo.

Mmoja wa waandamanaji wanaompinga anaripotiwa akisema:

“Sifurahii kabisa kwamba Putin anaingia tena kwa muhula wake wa nne au sijui ni wa tano. Nafikiri anashikilia nafasi hii kinyume cha sheria,”

Aidha, katika jiji la Moscow, Saint Petersburg na miji mingine kadhaa ya taifa hilo, hakukuwa na idhini ya maandamano na polisi ilitumia nguvu kuwatimua waandamanaji waliokiuka amri hiyo.

DW


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here