SHARE

Kocha mtarajiwa wa Yanga, Mkongo Mwinyi Zahera ameitoa timu hiyo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kutaka kutilia mkazo zaidi mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports itakayochezwa Jumatano ijayo.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wakitokea Algeria ilipokwenda kucheza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kuanza vibaya kwa kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa wenyeji wao USM Alger, kocha Zahera alisema kwa sasa haoni sababu ya kukimbizana na Simba katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara badala yake wanatakiwa kuwaza mechi ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa nyumbani.

Yanga kabla ya mchezo wa Rayon Sports ya Rwanda itakuwa na mechi mbili ngumu za Ligi Kuu ugenini kwanza watakwenda Mbeya kuifuata Tanzania Prisons Mei 10, kabla ya kurudi Morogoro kuwavaa Mtibwa Sugar Mei 13.

Mechi hizo mbili ndizo zitaamua hatma ya Yanga katika mbio za ubingwa msimu huu ambao watani zake Simba sasa wanahitaji pointi mbili tu au Yanga ipoteze mechi moja au sare kuwavua taji hilo.

Kocha huyo anayesubiri kutia saini mkataba, alisema kwa sasa ni vigumu kuizuia Simba kutwaa ubingwa hivyo ni busara kuangalia mashindano ya kimataifa.

Simba inahitaji pointi mbili kuwa mabingwa wapya wa ligi baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 65, wakiacha Yanga kwa pointi 17 kabla ya mechi za wiki hii dhidi ya Singida United.

Zahera alisema ameiona ratiba ya mechi za ligi za Yanga zilizosalia ni ngumu na haitoi afya kwa wachezaji wake kufanya vizuri kama itashindikana kubadilishwa ni lazima wagawanye kikosi chao.

“Hii ni ratiba ngumu kwetu leo (jana) tunarudi hapa, lakini tunatakiwa kesho (leo) tuanze safari kwenda Mbeya tukimaliza hapo turudi Morogoro na tukimaliza hapo tucheze na Rayon,” alisema Zahera.

“Sioni kama Yanga inaweza kufanya kitu tofauti katika ligi ya hapa Simba wanazidi kufanya vizuri wanataka kuwa mabingwa, sisi tunataka nafasi ya pili ni bora tuangalie mechi za kimataifa na sio ligi tena.

“Mpango wangu nimewaambia uongozi kama watashindwa kukubaliana na wakubwa wa mpira wa hapa (TFF), kubadilisha hii ratiba basi ni bora tukigawe kikosi baadhi wacheze mechi za ligi na wengine nibaki nao hapa tujiandae na mechi ya Rayon.”

Aidha Zahera alisema kipigo cha mabao 4-0 ilichopata Yanga inatokana na uzoefu mkubwa wa wapinzani wao USM Alger.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika alisema wamepangiwa ratiba ngumu wanataka kukutana na TFF kuangalia kuwezakano wa kubadilisha baadhi ya mechi.

“Tumeshakutana benchi la ufundi kuna maelekezo tumepewa kama uongozi kazi yetu ni kuyafanyia kazi, hii ratiba ni ngumu kutekelezeka kama tunataka ushindani wa kweli baina ya timu na timu, tutakutana na TFF kuongea nao waweze kutubadilishia,” alisema Nyika.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here