SHARE

ASIKWAMBIE mtu, waliosema kuwa fedha sabuni ya roho wala hawakukosea. Hivi mnajua kama Winga wa Simba Shiza Kichuya mkataba wake unaelekea ukingoni mwisho wa msimu na tayari kuna timu za ndani na nje ya nchi zimeshaanza kumnyatia?

Kichuya aliyesajiliwa Msimbazi misimu miwili iliyopita akitokea Mtibwa Sugar, nyota yake imekuwa iking’ara tangu atue katika kikosi hicho kwa misimu yote miwili na kulikuwa na hofu ya kutoa mkono wa bai ili kusepa Simba.

Tayari ilishaanza minong’ono kwamba jamaa alishawekewa mzigo wa maana mezani na mabosi wa Azam ili kwenda kutoa huduma kule Chamazi kwa msimu ujao, huku pia watani wa Yanga, Simba nao wakitajwa kumpigia hesabu kimya kimya. Kadhalika gazeti la Mwanaspoti linafahamu mbali ya Azam walioweka mzigo wa maana na Yanga kumnyatia, lakini ukweli ni kwamba tayari Kaimu Rais wa Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ ameshapokea ofa nyingine za kuhitajika Kichuya nje ya Tanzania.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kasi ya Bilionea Mohammed ‘MO’ Dewji kumwaga fedha za maana kwa nyota wa Msimbazi, imemfanya Kichuya kuamua kuzifungia vioo klabu zote zinazomtaka kwa sasa kwani akili yake aendelee kuzikoga fedha za bilionea huyo.

Mmoja wa watu wa karibu wa MO Dewji, amelidokezea gazeti la Mwanaspoti kuwa tayari bilionea huyo ameshaongea na Kichuya na mazungumzo yao yamefikia katika hatua nzuri.

“Tunafahamu Azam wameweka pesa nzuri ya kumtaka Kichuya, lakini hata Yanga taarifa zao tunazo kwa upande wetu hatuna wasi wasi wowote na Kichuya na hawezi kwenda katika hizo timu mbili,” alisema mtu huyo wa karibu aliyeomba kuhifadhiwa jina lake kwa sasa. “MO alifanya kikao cha muda mfupi na Kichuya na kumueleza atampatia pesa nzuri pindi atakapoongeza mkataba mpya ndani ya Simba.

“Kichuya baada ya kikao hicho alitoa jibu kuwa kama Simba watashindwa kumpa pesa ambayo watakubaliana basi hatasaini timu yoyote hapa Bongo,” alisema kigogo huyo wa Simba.

Kichuya mwenyewe alipotafutwa kufafanua juu ya taarifa hizo na kuamua kukaushia michongo mingine, alisema kwa ufupi;“Sitasaini mkataba na timu yoyote mpaka mkataba wangu na Simba utakapomalizika.”


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here