SHARE

Zilianza kama tetesi, lakini baadaye zikahibitishwa na Mkuu wa Magereza wa Dar es Salaam kuwa Elizabeth Michael, aliyekuwa anatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani, sasa yuko nje; atatumikia kifungo kwa kufanya kazi za kijamii.

Elizabeth, maarufu kwa jina la Lulu ambaye alikuwa ameanza kuibukia katika uigizaji filamu, alipatikana na hatia ya kumuua bila ya kukusudia gwiji wa filamu nchini, Steven Kanumba.

Lulu, ambaye aliingia gerezani Novemba 13 mwaka jana, ametoka siku chache baada ya msanii mwingine nyota wa rap, Joseph Mbilinyi “Sugu” kutoka kwa msamaha wa Rais, na ikiwa miezi kadhaa baada ya wanamuziki wa dansi, Nguza Vicking na mwanae, Papi kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais.

Lakini Lulu hakuwa na sifa za kupata msamaha na hivyo atapangiwa kazi za kijamii, ambazo mara nyingi huhusisha shughuli kama usafi katika majengo ya Serikali au ushauri kwa jamii.

Kutoka kwake kumeacha bumbuwazi uraiani ambako ndugu, jamaa na marafiki zake wa karibu jana hawakutaka kuzungumzia suala hilo na wala kueleza aliko msanii huyo aliyeng’ara katika filamu ya Woman of Principles na Mapenzi ya Mungu.

Taarifa za kuachiwa kwa Lulu zilizagaa kwa kasi jana na baadaye gazeti la Mwananchi ilimpata mkuu wa Magereza wa Dar es Salaam, Augustine Mboje aliyeeleza jinsi Lulu alivyobadilishia adhabu na Mahakama Kuu.

“Ieleweke kwamba Lulu hajamaliza kifungo. Bado ataendelea kutambulika kama mfungwa,” alisema Mboje.

Mboje, ambaye ni Naibu Kamishna wa Magereza alisema kwa mujibu wa taratibu, Lulu alitakiwa kumaliza kifungo chake Machi 12 mwakani, endapo asingebadilishiwa adhabu ya kifungo gerezani na kuwa kifungo cha nje.

Alisema kwa kuwa Magereza ina utaratibu wa kutoa msahama wa theluthi moja ya kifungo, msanii huyo alinufaika baada ya kuonyesha tabia njema.

Hata hivyo, Mboje alisema Lulu alinufaika pia na msamaha wa Rais John Magufuli uliotolewa Aprili 26 katika maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hata hivyo, haikuwezekana Lulu kutoka moja kwa moja siku hiyo kwa kuwa alikosa sifa ya kutumikia robo ya kifungo chake cha miaka miwili.

“Endapo Lulu asingetoka kwa sheria ya huduma ya jamii, angetolewa Novemba 12 mwaka huu baada ya kupata msamaha wa rais,” alisema Mboje.

Alisema kazi na huduma atakazokuwa akitoa Lulu zitasimamiwa na maofisa wa huduma za jamii, ambao pia watampangia muda wa kuanza kufanya kazi na kumaliza.

Mboje alisema Lulu anaweza kurudi gerezani na kumalizia kifungo chake endapo atabainika kukiuka masharti aliyopewa na maofisa wa huduma za jamii watakaokuwa wakimsimamia.

Alisema Lulu alitolewa gerezani Jumamosi asubuhi.

Lakini ni Mboje pekee aliyekuwa tayari kuzungumzia suala la Lulu.

Juhudi za gazeti la  Mwananchi kuongea na mama yake, hazikufanikiwa baada ya mzazi huyo kukata simu.

“Nani mwenzangu,” aliuliza mama yake Lulu, na baada ya mwandishi kujitambulisha, alikata simu.

Mpenzi wa Lulu, Francis Shiza ambaye anajulikana zaidi kama Majizo, naye hakutaka kuzungumzia suala hilo, akidai kuwa alikuwa kikaoni tangu asubuhi.

Msanii mwenzake, Muhsin Awadh, maarufu kama Cheni ambaye hujitambulisha kama mlezi wa Lulu, pia hakutaka kuzungumzia kuachiwa kwa nyota huyo.

“Nashindwa kusema lolote kwa sasa, habari za Lulu kupewa kifungo cha nje nimezisikia leo kupitia mitandao ya kijamii ambayo huwa siiamini. Nashindwa kukuambia nimezipokeaje kwa sababu sijapata uhakika,” alisema Cheni.

“Nimejaribu kuwasiliana na mama Lulu simpati kwa simu. Nimepatwa na mshituko na siamini nilichosikia kuhusu Lulu kupewa kifungo cha nje.”

Mwishoni mwa mwaka jana baada ya Rais John Magufuli kutangaza msamaha uliowahusisha Nguza na mwanae, waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kubaka wanafunzi, Jeshi la Magereza lilisema Lulu hakunufaika na msamaha huo kwa kuwa aliingia gerezani wakati mchakato wa kufuatilia wanaostahili msamaha ukiwa umeshapita.

“Msamaha huu (wa Desemba 9, 2017) haukumuhusu yeye (Lulu) kwa sababu aliingia magereza wakati tayari zoezi hili lilikuwa limekamilika. Kwa hiyo labda misamaha ijayo kama itakuwepo, lakini huu haukumuhusu,” alisema Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa alisema wakati huo.

Mama Kanumba aanza maombi

Lakini taarifa za kutoka kwa Lulu hazikuwa njema kwa mama yake Kanumba anayeitwa Flora Mtegoa aliyesema ameumia na alikosa usingizi usiku wa kuamkia jana baada ya kupata taarifa hizo.

“Nimeamua kwenda kwenye maombi kwa ajili ya afya yangu nisije kupata presha. Najisikia vibaya sana,” alisema.

“Ingawa si mimi niliyemuhukumu, huyo binti alipaswa kukaa hata mwaka mmoja ili roho yangu iridhike. Lakini ndio hivyo, maskini sina haki.”

Hata hivyo aliwashukuru wote waliohusika kumtoa. “Lakini yote namuachia Mungu.”

Wakati Mama Kanumba akisononeka, habari za kuachiwa kwa Lulu zilifurahisha wasanii wenzake, huku kiongozi wao, Steve Nyerere akionya mwenendo wa mcheza filamu huyo na waburudishaji wengine.

“Tusisahau hili, wengi hawakujua. Tunapomzungumzia Lulu ni sterling (mwendesha) wa familia; ndiyo baba na mama,” alisema Steve.

“Anapoondoka familia inatetereka kidogo. Kifungo cha nje kwa mwenzetu kitamsaidia kuwa karibu na wa kwao.”

Lakini Steve akawataka vijana na wasanii kulichukulia suala la Lulu kama ni funzo hivyo wajifunze jinsi ya kuishi katika jamii inayowazunguka.

“Tunaishukuru Mahakama Kuu ya Tanzania kwa maamuzi mazuri. Nina imani atatimiza majukumu yake ya kifungo cha nje kama alivyoelekezwa,” alisema.

Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema tukio la msanii huyo linaonyesha dhahiri kuwa sheria ipo, hivyo wasanii hawana budi kuifuata.

“Tumejua kwamba sheria ni msumeno na inakata kote. Maoni yangu ni wasanii kama kioo cha jamii, tuishi maisha ambayo hayatatuingiza katika mtego kama wa Lulu,” alisema.

Novemba, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema Lulu aliingia katika mahusiano akiwa bado mdogo, lakini hata hivyo kuna kila sababu kwa wasanii kuona uthamani wa ndoa na kuingia katika maisha hayo ili kuepuka matatizo yanayoweza kuepukika.

Alisema gereza ni sehemu ambayo wanafundishwa maadili, hivyo anatarajia Lulu atakuwa mfano katika kupambana na kuieleza jamii kuhusu nini amejifunza kwa kuwa mtu yeyote anaweza kwenda jela.

Msanii mwingine wa filamu, Wema Sepetu aliweka picha ya Lulu na kuandika maneno mafupi “Wellcome (welcome?) back baby”, huku Malaika akiweka ujumbe ulioambatana na picha, akisema: “Na kwa sababu Mungu wetu ni wa wote na yeye anafanya kwa wakati wake.”


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here