SHARE

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 15 (2) inasema “ kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo

isipokuwa (a) katika hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au (b) katika kutekeleza hukumu, amri au adhabu iliyotolewa na mahakama kutokana na shauri au na mtu kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.”

Tafsiri ya ibara hii ni kuwa hairuhusiwi kwa mtu yeyote au chombo chochote kunyang’anya uhuru wa mtu kuwa huru (kukamata) kinyume na njia zilizoainishwa na sheria zetu za nchi au wakati wa kutekeleza amri ya mahakama.

Busara ya ibara hii ni kutoa fursa kwa kila mtu ndani ya nchi kupata nafasi ya kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo yake binafsi na yale ya kijamii kwa uhuru wa kwenda mahali popote bila kuzuiwa au kupata kizuizi chochote.

Ni vigumu kwa mtu kushiriki katika shughuli za maendeleo kama hayuko huru au amezuiwa kwenda mahali popote anakoona kunafaa kujipatia riziki.

Kwa maana hii, ni lazima ziwepo taratibu za kisheria ambazo zinapaswa kufuatwa wakati wa kuiondoa haki hii.

Tuna wajibu wa kuepuka kufanya makosa ambayo yatatufanya tukamatwe na kuondolewa haki hii ya kikatiba ya kuishi kama mtu huru. Hata hivyo, pamoja na kwamba tunaweza kujitahidi kuepuka kufanya makosa, maisha nayo hayatabiriki.

Yumkini unaweza kukamatwa kimakosa au likatokea jambo lolote lisilotarajiwa litakalokufanya ukamatwe.

Na hata usipokamatwa, yumkini mtu yoyote wa karibu kama rafiki, ndugu au jirani anaweza kukamatwa. Kimsingi, kukamatwa ni jambo linaloweza kumtokea mtu yoyote.

Kwa maana hii, ni muhimu kupata taarifa za kutosha zinazohusiana na kukamatwa. Taarifa hizi zitakupa muongozo wa kujua haki na wajibu wako pale unapokamatwa au mtu wako wa karibu anapokamatwa.

Kwa maana hii, yafuatayo ni baadhi ya mambo ya msingi ya kufahamu pale mtu yoyote anapokamatwa.

MAANA YA KUKAMATWA

Kumkamata mtu kwa mujibu wa sheria ni kitendo cha kumuondolea mtu uhuru wake wa kufanya harakati zake za kila siku kwa kumpeleka kwenye kizuizi kinachotambulika kisheria.

Mtuhumiwa anawekwa kizuizini ili apelekwe mahakamani (mapema kwa kadri itakavyowezekana) kujibu mashtaka ya jinai yanayomkabili.

Anaweza pia kuwekwa kizuizini kwa lengo la kufanyiwa upelelezi juu ya mashtaka ya jinai yanayomkabili.

JINSI YA KUMKAMATA MTUHUMIWA

Sura ya 20 ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ndiyo sheria inayotoa mwongozo wa namna na jinsi ya kumkamata mtu.

Kwa kawaida, kukamatwa kunahusisha kugusa au kumshika mtuhumiwa kwa namna itakayomfanya ashindwe kumtoroka au kumkimbia mtu aliyemkamata.

Kama mtu anayekamatwa atajaribu kukimbia au kufanya jaribio la kuzuia tendo la ukamatwaji halali kufanyika, mtu au afisa anayemkamata anaruhusiwa kutumia nguvu kiasi.

Ukamatwaji haupaswi kuendeshwa kwa maslahi binafsi bali unatakiwa kufanywa kwa nia njema ukizingatia utu, usiri na haki za binadamu. Mkamataji anapaswa kutanguliza maslahi ya kutenda haki wakati anamkamata mtuhumiwa.

AINA ZA UKAMATAJI

Kuna aina mbili za ukamataji. Kumkamata mtu kwa kutumia kibali na kumkamata mtu bila kutumia kibali. Ukamatwaji unaotumia kibali kwa kawaida unatolewa na hakimu, katibu kata au katibu wa halmashauri ya kijiji baada ya kupokea taarifa iliyo chini ya kiapo ikimtuhumu mtuhumiwa kuwa kuna sababu za msingi za kuamini kuwa mtu husika ametenda kosa.

Ukamatwaji usio na kibali ni ukamatwaji unaofanywa pale makosa kama uvunjifu wa amani mbele ya polisi au hakimu yanapotokea, kumzuia afisa polisi kutekeleza majukumu yake au kitendo chochote kinachoazimia kutusi nembo ya taifa au bendera ya taifa.

SABABU ZA MTU KUKAMATWA

Polisi au afisa anayemkamata mtuhumiwa ana wajibu wa kutaja kosa au kutoa sababu zinazomfanya amkamate mtuhumiwa.

Ieleweke kuwa sio kila kosa linaweza kukufanya ukamatwe (na hasa makosa ya madai). Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazoweza kumfanya mtu akakamatwa.

Kwanza, makosa ya jinai kutegemeana na aina au uzito wa kosa ambalo mtuhumiwa ametuhumiwa kulifanya. Endapo mtuhumiwa atadhaniwa kufanya kosa la ugaidi, uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha na makosa mengineyo ya jinai, yatamfanya akamatwe mara moja.

Sababu ya pili inayoweza kumfanya mtu akamatwe ni kudharau kutii amri halali ya mahakama au kukwepa kwa makusudi kufikiwa na wito wa kufika mahakamani.

Yumkini mtuhumiwa ameitwa mara kadhaa mahakamani au amekataa kupokea wito, basi mtuhumiwa anaweza kukamatwa kwa kosa hili.

Ulinzi wa uhai na usalama wa mtuhumiwa inaweza kuwa sababu ya tatu itakayomfanya mtu akamatwe. Mtuhumiwa anaweza kufanya tukio linaloweza kuibua hasira kali kwenye jamii na hivyo wananchi wakataka kuchukua hatua mkononi.

Kama polisi amejiridhisha kuwa uhai wa mtuhumiwa uko hatarini, mtuhumiwa anaweza kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda ili kulinda uhai na usalama wa maisha yake.

Sababu ya nne inayoweza kumfanya mtu kukamatwa ni pale usalama wa jamii na watu wengine unapokuwa hatarini. Yumkini mtu husika ana matatizo ya akili au ni mtu anayependa kufanya vurugu, kuharibu mali na kujeruhi watu.

Polisi na viongozi wa maeneo husika wakijiridhisha kuwa anavyoendelea kuwa uraiani atazidi kufanya uharibifu nayo inaweza kuwa ni sababu ya kumkamata mtu husika.

Lengo la ukamatwaji huu ni kumdhibiti mtu husika asiendelee kufanya uharibifu.

UKAMATAJI KINYUME CHA SHERIA

Ukamatwaji ulio kinyume na sheria ni ule ukamataji unaofanywa kinyume na vipengele vya kisheria vilivyopo kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai vinavyoelekeza namna na jinsi ya kumkamata mtuhumiwa.

Ukamatwaji ulio kinyume na sheria unahusisha mambo yafuatayo; Kumkamata mtu bila kuwa na mamlaka ya kisheria, kumkamata mtu bila kumtaarifu sababu za kumkamata, na kutumia nguvu kubwa (zilizopitiliza).

Aidha, kumkamata mtu bila sababu za msingi, kumuweka mtuhumiwa kizuizini kwa muda mrefu tofauti na mahitaji ya kisheria yanavyotaka.

Mtuhumiwa anatakiwa apelekwe mahakamani ndani ya saa 24 au kuachiwa kwa dhamana. Vitendo vya kikatili au vitendo vilivyo kinyume na haki za binadamu wakati wa ukamatwaji navyo haviruhusiwi kwa mujibu wa sheria.

Yapo madhara kwa polisi au afisa kumkamata mtuhumiwa kwa namna iliyo kinyume na sheria. Mtu aliyekamatwa kinyume na sheria anaweza kumshtaki afisa husika kwa kosa la shambulizi, matumizi mabaya ya mamlaka ya kipolisi, au afisa husika kuadhibiwa kitaaluma kwa kufanya makosa ya kinidhamu (professional misconduct).

Kama mtuhumiwa amekamatwa kimakosa au hakuna sababu ya msingi ya kuendelea kumshikilia, basi anapaswa kuachiwa mara moja. Vinginevyo anapaswa kupewa dhamana au kupelekwa mahakamani (iliyo karibu na kituo) ndani ya saa 24 baada ya kukamatwa kwake kama inavyoelekeza Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 33.

Endapo mtuhumiwa ataendelea kushikiliwa kwa zaidi ya saa 24 bila kupelekwa mahakamani, basi upande wa mshitakiwa utaomba agizo la kimahakama litolewe (habeas corpus) ili mtuhumiwa aweze kupelekwa mahakamani kama sheria inavyoelekeza.

Barua pepe; fransiscompangala08@gmail.com


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here