SHARE

Mabao mawili aliyofunga nahodha na mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta dhidi ya Charleroi yameweka hai matumaini ya KRC Genk kushiriki michuano ya Europa League msimu ujao.

KRC Genk wameibuka na ushindi wa mabao 4-1 mbele ya Charleroi kwenye mchezo wa tisa wa mchujo daraja A, uliochezwa jana usiku Cristal Arena.

Mshambuliaji huyo aliyekuwa na ukame wa mabao akishindwa kufunga kwenge mechi 16 amefunga mabao matatu ndani ya mechi mbili yakiwemo hayo mawili aliyofunga dakika ya 24 na 61.

Ushindi huo kwa Genk umeifanya kufikisha pointi 35 zilizowasogeza nafasi ya 5 kutoka 6, huku wakisaliwa na mchezo mmoja watakaocheza Mei 20 dhidi ya Anderlecht, ugenini.

Kama Genk wataifunga Anderlecht ambayo ipo nafasi 4 na pointi 36 na wakipoteza kwa Club Brugge ambayo inawania ubingwa wa ligi, klabu hiyo ya Samatta itaingia moja kwa moja hatua ya makundi Europea League.

Lakini, wakipoteza na kusalia kwenye nafasi ya tano watacheza mchujo mwingine ili kupigania nafasi ya kuingia makundi na mshindi wa daraja B.

Wabelgiji wanacheza ligi kuu kwenye sura nne, sura ya kwanza na ya pili ni duru la kwanza na pili, baada ya hapo wanaingia kwenye sura ya tatu na nne.

Sura hizo ni mgawanyo wa makundi mawili kundi la timu sita za juu zinaunda ligi ambayo huitwa daraja A yenye duru lingine la kwaza na pili ili kupata bingwa na washiriki wa michuano ya Ulaya msimu ujao.

Waliosalia nao hucheza kwa namna hiyo ili kupata timu zitakazo shuka daraja na ile itakayofanya vizuri itacheza mchujo na atakayeshika nafasi ya tano daraja A ili kushiriki Europa League.

Anayemaliza nafasi ya kwanza daraja A anachukua ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki Uefa msimu ujao wa nafasi ya pili atacheza hatua ya awali na nafasi tatu na nne wanaingia moja kwa moja hatua ya makundi Europa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here