SHARE

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema itambana Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba kwa hoja tano atakapowasilisha bajeti ya wizara yake bungeni jijini Dodoma leo.

Ratiba ya mkutano wa Bunge la Bajeti iliyotolewa na Idara ya Habari na Elimu ya Bunge, inaonyesha kutakuwa na mjadala wa siku mbili wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kuanzia leo.

Akizungumza na gazeti la Nipashe jijini hapa jana, Naibu Waziri Kivuli wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Immaculate Sware, alizitaja hoja hizo kuwa ni pamoja na kupunguzwa kwa fedha za maendeleo za miradi ya kilimo na upungufu wa watumishi katika sekta hiyo.

Alisema hoja nyingine ni uhaba wa pembejeo za kilimo, serikali kutokuwa na mkakati wa kufunganisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda pamoja na udhibiti wa mazao baada ya kuvunwa.

Akifafanua hoja hizo, Dk. Sware alisema fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Hazina kwa ajili ya kilimo, zimekuwa zikipungua kila mwaka na kusababisha athari hasi kwa Watanzania ambao kwa zaidi ya asilimia 70 wanategemea rasilimali ardhi kwa shughuli za kilimo.

“Serikali pia haijaweka mikakati ya wazi ya kufungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda na nchi bado ina uwekezaji mdogo kwenye kilimo,” alisema na kuongeza:

“Kuna uhaba, ucheleweshaji, ubora hafifu na bei ya juu ya pembejeo katika baadhi ya maeneo huku pia kukikosekana mfumo thabiti wa kuzuia pembejeo zisizo na ubora kwenye soko,” alisema.

Dk. Sware alisema watautumia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kuibana serikali kuhusu upungufu wa watumishi katika sekta ya kilimo, akibainisha kuwa kuna upungufu wa asilimia 45 wa wataalamu na maofisa ugani.

“Pia wachache waliopo wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi,” alisema.

Dk. Sware ambaye kabla ya kuwa mbunge, alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema wamepanga kuutumia mjadala huo kuibana serikali ili iongeze maghala ya kuhifadhi chakula.

Alibainisha kwa sasa kuna takriban maghala 1,200 wakati nchi ina zaidi ya vijiji 13,000 huku pia nchi ikikabiliwa na changamoto ya teknolojia duni katika uvunaji na usindikaji wa mazao.

“Hii inasababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Asilimia 30 ya mazao nchini hupotea baada ya mavuno. Ukirejea kitabu cha Mpango wa Taifa wa Maendeleo, unaona kabisa kilimo si kipaumbele cha serikali,” alisema


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here