SHARE

TANZANIA imekubaliwa kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 ya thamani ya bidhaa za mitumba ya nguo na ngozi, inayotoka nje ya Afrika Mashariki.

Bunge pia limeelezwa kuwa Tanzania imekubaliwa kuendelea kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa sukari ya viwandani, inayoingizwa nchini kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage sukari ya majumbani kutoka huko inatozwa ushuru wa asilimia 25. Ushuru kwenye mitumba Waziri Mwijage alisema, Tanzania inatoza ushuru mitumba kutokana na kusudio la Marekani kutaka kuziondoa nchi za Rwanda, Tanzania na Uganda kwenye mpango wa Sheria ya Ukuaji na Fursa kwa Afrika (AGOA).

Kwa mujibu wa Mwijage, wakati wa mkutano wa dharura wa 35 wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki uliofanyika jijini Kampala, Uganda Februari 15-20 mwaka huu, Wizara hiyo iliomba na kukubaliwa kutoza ushuru huo. Alisema, Marekani iliamua kuzitia nchi hizo kwenye mpango wa AGOA kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki ziliongeza kodi kwenye bidhaa za mitumba zikiwemo nguo na viatu kutoka Dola senti 20 hadi Dola senti 40 kwa kilo moja na kutoza kodi ya asilimia 35 ya thamani ya bidhaa. “Hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kuendelea kunufaika na fursa za soko la AGOA,” alisema Waziri Mwijage.

Alisema, kwa mwaka 2017 mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Marekani kupitia AGOA yaliongezeka hadi Dola za Marekani milioni 40.545 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 37.476 mwaka 2016. Kwa mujibu wa Mwijage, mauzo hayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na sekta ya nguo na mavazi kwa asilimia 99.2. Ushuru wa sukari Waziri Mwijage aliwaeleza wabunge kuwa, wakati wa mkutano wa 29 wa Kamati ya Mawaziri wa Biashara wa SADC uliofanyika Pretoria, Afrika Kusini Agosti 14, mwaka jana, Tanzania ilifanikiwa kutetea na kukubaliwa kuendelea kutoza ushuru sukari ya viwandain na majumbani inayotoka nchi za SADC.

Wabunge walielezwa kuwa ushuru huo utatozwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2019/2020. “Vilevile muktano huo uliridhia maombi ya Tanzania ya kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za karatasi za vifungashio zinazoingizwa nchini kutoka nchi za SADC kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2019/2020,” amesema Waziri Mwijage. Alisema ushuru huo una lengo la kulinda na kutoa fursa kwa viwanda vya sukari na karatasi nchini, kujipanga kuhimili ushindani kutoka kwa wazalishaji katika soko la SADC.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here