SHARE

Nyota na nahodha wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia anatarajiwa kutua nchini Juni 20 ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki kuinoa timu ya Taifa ya vijana ya Serengeti Boys inayojiandaa na mashindano ya mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana.

Hyypia atatua nchini katika ziara ya siku tatu iliyoratibiwa na benki ya Standard Chartered ambayo ni wadhamini wa klabu ya Liverpool inayoshiriki Ligi Kuu England.

Akizungumzia ziara hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani alisema nyota huyo atakuwa nchini kwa siku tatu na Juni 23 atashuhudia mchuano wa kombe la Standard Chartered itakayofanyika nchini.

Michuano hiyo maarufu kama Watch Liverpool FC live at Anfield itashindanisha timu 32 za nchini ambapo bingwa atapata nafasi ya kucheza kwenye uwanja wa Liverpool katika mashindano ya dunia ya kombe la Standard Chartered nchini Uingereza.

“Tofauti na miaka mingine, msimu huu ni tofauti kwani hatutakuwa na timu za Kenya na Uganda, hivyo mshindi wa Tanzania atakwenda moja kwa moja Uingereza kushiriki mashindano ya dunia ya kombe la Standard Chartered pale Anfield,” alisema Rughani.

Alisema katika fainali ya Taifa itakayofanyika Dar es Salaam, itashuhudiwa na Hyypia ambaye atafanya mambo mengine ya kimichezo ikiwamo kuinoa Serengeti Boys sanjari na kuzungumza na wateja wa benki hiyo.

“Maandalizi ya ujio wake na mashindano ya Kombe la Standard Chartered yanaendelea vizuri na uandikishaji wa timu shiriki utaanza mapema wiki hii,” alisema.

Alitaja vigezo vya kushiriki kuwa ni lazima timu iwe mdau wa benki hiyo.

“Kila timu itakuwa na wachezaji saba ambao watano watakuwa wa kikosi cha kwanza na wawili wa akiba, timu itakayoibuka bingwa wachezaji wote saba watagharamiwa usafiri na malazi kwenda Uingereza kushuhudia moja ya mechi za Liverpool,” alisema Rughani.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo alisema ujio wa Hyypia ni nafasi ya pekee kwa timu hiyo ya vijana ambayo itaiwakilisha nchi kwenye AFCON ya vijana mwakani.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here