SHARE

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi jana alikataa kukaa eneo alilotengewa kama mgeni rasmi akidai kuwa hawezi kukaa kivulini wakati wanafunzi wamekaa juani.

Dk Nchimbi alichukua uamuzi huo wakati akizindua wiki ya elimu inayofanyika kitaifa wilayani Mkalama mkoani hapa.

Ilikuwa ni baada ya kupokea maandamano ya shule mbalimbali wilayani humo na kuona watoto wote wakiwa wamesimama juani.

“Mimi ni mama, mimi ni mwakilishi wa Serikali siwezi kukaa kivulini halafu niwaangalie watoto wako juani kwa hiyo watu wote wa meza kuu tushuke kwenye jua,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Serikali ina upendo na huruma kwa watoto na Watanzania, haiwezekani watu wazima wakae kivulini watoto wakae juani.”

Baada ya kauli hiyo watendaji, viongozi wa Serikali na wadau wa elimu ambao walikuwa wamekaa jukwaani walishuka chini na kuhamishia viti vyao juani.

Katika hafla hiyo, Dk Nchimbi alipokea maandamano ya wanafunzi wakiwa na mabango mbalimbali yenye ujumbe kuhusu elimu.

Akizungumzia kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani Mkalama, Dk Nchimbi alisema Serikali itaongeza kiwango cha fedha kwa ajili ya elimu bure na mwaka huu tayari wamepokea Sh15 bilioni.

“Nataka niwambie Serikali ipo na inafanya kazi kwa nguvu zote mwaka 2016 wanafunzi wa awali walioandikishwa walikuwa 44,569 ila mwaka huu wameandikishwa 60,869.

“Darasa la kwanza mwaka 2016 waliandikishwa 43,840 na mwaka huu ni 68,981,” alisema.

Naye mratibu wa Mtandao wa Elimu (Tenmet), Cathleen Sekwao alisema uamuzi wa kufanya maadhimisho hayo wilayani Mkalama ni kwa sababu haikufanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba mwaka jana.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here