SHARE

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wikiendi hii anatarajiwa kuwasili nchini Uganda siyo kwa ziara rasmi ya kikazi bali kutoa mahari ya ng’ombe 100 na zawadi nyingine kwa ajili ya kijana wake Andile.

Binti ambaye mahari itatolewa kwa ajili yake ni Rwakairu Bridget, ambaye pia ni mpwa wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uganda na mgombea urais Amama Mbabazi.

Bridget, mwenye umri wa miaka 37 ni mtoto wa hayati Shadrack Rwakairu wa Kabale na Peace Ruhindi, dada wa Jacquieline ambaye ni mke wa Mbabazi.

Binti huyo aliyesoma Shule ya Msingi ya Nyakisoroza ana shahada ya uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) aliyohitimu katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Beijing, China. Pia, ana shahada ya kwanza ya Uhandisi wa Mazingira aliyoipata Chuo Kikuu cha Jiatong Beijing.

Katika majukumu yake kama baba, mkuu huyo wa nchi ya Afrika Kusini ataongoza msafara wa ndugu, jamaa na marafiki wa karibu kutoka Johannesburg hadi Kampala.

Taarifa ya familia ya Bridget kwa vyombo vya habari kuhusu ugeni huo imesema sherehe hizo za kitamaduni zitafanyika Kololo, nje kidogo ya jiji la Kampala.

Orodha ya wageni ilibaki kuwa siri ingawa usalama umeimarishwa kutokana na kusubiriwa viongozi wa kitaifa, wageni waheshimiwa na wanasiasa wa ngazi ya juu kutoka Kampala na Johannesburg.

“Kwa kuzingatia mila na desturi, ndoa lazima itanguliwe na sherehe za kitamaduni ambazo zinafahamika kama ‘Okhusaba’ na zitafanyika Mei 19. Sherehe zitafanyika kwenye viunga vya 10 Nyanyi Gardens huko Kololo, nyumbani kwa Amama Mbabazi,” ilisema taarifa ya familia ya Mbabazi.

Huko ndiko Ramaphosa atakabidhi ng’ombe hao na zawadi nyingine kwa familia ya Mbabazi kama alama ya shukrani kwa kumlea vizuri binti.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here