SHARE

Serikali ya Guinea ilijiuzulu Alhamisi kabla ya siku iliyopangwa kufanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na pia siku moja baada ya vyama vya upinzani kusitisha maandamano dhidi ya mzozo wa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Waziri Mkuu Mamady Youla aliwasilisha barua yake pamoja na ya serikali nzima, amesema waziri wa nchi na msemaji wa rais, Kiridi Bangoura.

Bangoura aliviambia vyombo vya habari kwamba serikali iliyomaliza muda wake itasalia madarakani kwa shughuli za kila siku hadi serikali mpya itakapotangazwa.

Alpha Conde, mpinzani wa kihistoria ambaye aliingia madarakani mwaka 2010 aliahidi kuwasikiliza “wafuasi wengi wasioshiriki vurugu” na kuendelea na “mabadiliko makubwa ya mawaziri” ili “kuwateua mawaziri wanaosikiliza kero za watu na wanaosimamia programu zao.”

Jumatano, vyama vya upinzani vilisitisha maandamano ya mitaani yaliyoandaliwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Februari wakisema jumuiya ya kimataifa imejitolea kupatanisha.

Chama cha Rally of the Guinean People (RPG) cha Conde kiliushinda muungano wa upinzani ulioongozwa na Union of Democratic Forces of Guinea (UFDG).

Jumatatu, upinzani ulifanya maandamano makubwa na kusababisha shughuli za kibiashara na usafiri kuvurugika katika baadhi ya Jiji la Conakry.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here