SHARE

Rais Donald Trump amempa hakikisho Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un la kuendelea kuwepo madarakani endapo tu ataachana na silaha za nyuklia lakini akiendelea kukaidi yanaweza kumfika yaliyomkuta kiongozi wa zamani wa Libya.

Katika juhudi za kuhakikisha mkutano wa kilele uliopangwa kumkutanisha na Kim mwezi ujao, Trump alisema Alhamisi kwamba Korea Kaskazini “itapata ulinzi madhabuti” endapo mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa na kwa mafanikio.

“Atabaki nchini kwake na ataendelea kuongoza nchi. Nchi yake itakuwa tajiri,” aliwaambia waandishi wa habari.Lakini ahadi hiyo iliwekewa uzio ikiwa mazungumzo yatashindikana, Kim anaweza kukabiliwa na mkasa uliomkuta Muammar Gaddafi kupinduliwa madarakani na waasi na hatimaye kuuawa kikatili.

Mkasa uliomkuta Gaddafi unaonyesha “kitakachotokea ikiwa hatutafikia makubaliano,” ameonya Rais huyo wa Marekani.

Kauli ya Trump imekuja baada ya Korea Kaskazini kutishia kujiondoa na kufuta mkutano wa kihistoria baina ya viongozi wawili hao uliopangwa kufanyika Juni 12 Singapore akilalamikia matakwa ya Marekani ya “kuachana moja kwa moja na silaha za nyuklia.”

Ofisa mmoja wa Korea Kaskazini pia amekejeli maoni yaliyotolewa na mshauri wa usalama wa Trump John Bolton kwa kuyaita “upuuzi” alipoitaja Libya kuwa mfano mzuri wan chi iliyoachana na silaha za nyuklia.

Mfano ambao Bolton alikuwa akiuzungumzia ni ule mkataba wa mwaka 2003 ambao Gaddafi alikubali kuachilia mbali programu ya nyuklia na siala za kemikali ili aweze kupata unafuu wa vikwazo alivyokuwa amewekewa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here