SHARE

Familia ya kifalme nchini Uingereza imeandika historia nyingine kwa kijana wao Harry kufunga pingu za maisha na Meghan Markle katika tukio lililofuatiliwa na watu zaidi ya milioni mbili duniani huku wawili hao wakimwaga machozi ya furaha.

Meghan alitumia gari aina ya Rolls Royce Phantom kufika kanisa la Mtakatifu George huku akisindikizwa na wavulana wawili wadogo walioandaliwa kunyanyua shela la bibi harusi.

Umati mkubwa wa watu uliokuwa umesimama kando ya barabara za jiji la London ulilipuka kelele za shangwe na kuonyesha kila aina ya furaha wakati Meghan alipokuwa akielekea kanisani. Alipofika kanisani alipokelewa na baba mkwe, mwanamfalme Charles aliyemsindikiza na kumkutanisha na mumewe mtarajiwa, Harry.

Sura za wawili hao zinaonyesha msisimko wa furaha na kila mara walionekana kutabasamu na kucheka.

Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby aliwaongoza wawili hao kula kiapo cha ndoa wakisema kuwa: “kwa mema, kwa mabaya, kwa utajiri, kwa umaskini, kwa ugonjwa na kwa afya, kukupenda na kukuenzi, hadi kifo kitutenganishe”.

Hata hivyo, katika sehemu ya kiapo chake Meghan hakutumia neno “kumtii” mume wake. Wakati Diana alipooana na Prince Charles mwaka 1981, aliondoa neno hilo kwenye kiapo na hilo likajitokeza kwenye harusi ya Prince William.

Muda mfupi kabla ya Harry (33) na Meghan (36) kufunga ndoa, Malkia Elizabeth ll wa Uingereza aliwapa wadhifa wa Duke na Duchess wa Sussex, ikimaanisha wana cheo chini ya mfalme.

Askofu Michael Curry aliyehubiri kwenye ibada ya harusi ndiye aliyesisimua zaidi kutokana na hotuba iliyogusia maana halisi ya upendo.

Curry anayeongoza kanisa la Kianglikana la Marekani, alinukuu baadhi maneno ya mwanaharakati wa zamani wa haki za raia wa Marekani, Martin Luther King, na kusema upendo umebeba dhamana kubwa katika maisha ya binadamu.

“Kuna nguvu katika upendo. Msidharau hili. Yeyote ambaye amewahi kupenda anajua ninachomaanisha,: alisema askofu Curry ambaye raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika.

“Kunapokuwa na upendo hakika tunafanyiana mambo mema kama vile tupo katika familia moja. Kunapokuwepo na upendo tunatambua kuwa Mungu ndiye chimbuko letu sote na ni kaka na dada….watoto wa Mungu.

“Kaka zangu na dada zangu, hiyo ndiyo mbingu mpya, dunia mpya, ulimwengu mpya na familia mpya ya ubinadamu,” alisema.

Askofu huyo aliyechaguliwa kuongoza Kanisa la Anglikana mwaka 2015 aliongeza kusema; “ baada ya kueleza haya nitakaa chini lakini sasa ebu kila mmoja wenu afunge ndoa”.

Vionjo vya harusi

Harusi ya Harry na Meghan inatajwa kuwa ya aina yake katika historia ya harusi nyingi za kifalme nchini Uingereza, kutokana na kwenda kinyume na utamaduni wa harusi za familia ya kifalme Uingereza ambazo hufanyika katikati ya wiki.

Wawili hao walichagua wimbo wa “Stand By Me” ulioimbwa na Karen Gibson na kwaya ya Kingdom. Awali wimbo huo uliimbwa na Ben E. King aliyeutunga na kuandika mashairi.

Pia Harry aliamua kuvaa pete ya ndoa, kitu ambacho kaka yake, baba yake na babu yake hawakukifanya.

Pia, wawili hao waliamua kutumia lugha ya Kiingereza cha kisasa badala kile cha asili. Katika neno “thee (wewe)”, walitumia neno “You” na hivyo kuwapa nafua waongozaji ibada.

Harusi ya Malkia Elizabeth iliandaliwa Alhamisi wakati ile ya William ilifanyika Ijumaa.

Harusi hiyo ilihudhuriwa na mamia ya watu mashuhuri duniani, kama David Bekham na mkewe Victoria, nyota wa vipindi vya televisheni wa Marekani, Oprah Winfrey, mwanamuziki maarufu wa Uingereza, Elton John, mwigizaji wa Kimarekani, Idris Elba, mcheza tennis maarufu, Serena Williams na mwanamuziki James Blunt. Picha za televisheni zimemwonyesha pia, mpenzi wa zamani wa Harry, Chelsy Davy.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here