SHARE

Sherehe ya harusi ya Mwana Mfalme, Harry na Meghan Merkle ilifana juzi huku Harry akimmiminia sifa mke wake mpya.

Ndoa yao ilifungwa juzi Mei 19 katika kanisa la St Georges Chapel, Windsor na sherehe hiyo ilifanyika jioni eneo la Frogmore House, Windsor Great Park.

Mwana Mfalme Harry alisikika akimwambia Meghan, ‘Tunaunda timu bora kabisa’ na baadaye akaongeza na kumwambia, “Nasubiri kwa hamu kuishi na wewe sehemu ya maisha yangu yaliyobaki.’’

Katika sherehe hiyo, wanandoa hao wapya walifungua muziki kwa wimbo wa marehemu Whitney Houston, ‘I wanna dance with somebody’

Kwa kuwa mama yake Meghan ni Mmarekani mweusi, wimbo huo wa Whitney Houston uliipa sherehe hiyo ladha ya Kimarekani.

Wanandoa hao na wageni waalikwa waliburudishwa zaidi na mwanamuziki mkongwe, Elton John, aliyetumbuiza nyimbo zake nne ikiwamo ‘Your Song, Tiny Dancer, Circle Of Life na I’m Still Standing’

Elton John alitumbuiza mara baada ya Harry, kuwatazama wageni waalikwa na kuuliza; “Kuna yeyote anaweza kupiga piano hapa?”

Kaka yake Harry, Mwana Mfalme, William, alitoa neno la shukrani akimshukuru Meghan kwa kujiunga na familia hiyo na Meghan hali kadhalika, aliishukuru familia hiyo ya kifalme kwa kumkubali.

Wakati wote wanandoa hao walionekana kukumbatiana, wakati mwingine wakilia, wakicheka na kupigana mabusu mbele ya mamia ya wageni waalikwa akiwamo nyota wa soka wa zamani, David Bekham, Mcheza filamu, Idris Elba, Mtangazaji, Oprah Winfrey na Mcheza tenisi, Serena Williams.

Walikwenda ukumbini wakiwa na gari maalum la wazi, linaloendeshwa kwa umeme na lililopewa namba za usajili maalum zenye tarehe ya jana E190518.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here