SHARE

Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar kimetoa onyo kali kwa wanachama ambao ni wajumbe wa mkutano mkuu Taifa kutoshirikiana na waliowaita wasaliti wa chama hicho.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi, mkurugenzi wa habari uenezi na uhusiano wa umma upande wa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Salim Bimani alisema wameshatoa tamko kuwataka wajumbe wa mkutano mkuu Taifa kukataa kurubuniwa ili kushiriki mkutano huo.

Bimani alisema tayari wana tetesi kuwa mkutano huo unaratibiwa na CUF Lipumba.

Alisema chama chao kina wajumbe wa mkutano mkuu halali kupitia mabaraza ya wilaya upande wa bara na visiwani.

“Hapa nataka niweke wazi hatutamvumilia mwanachama yeyote yule ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu Taifa kuona anashirikiana na Lipumba na kundi lake, ndiyo maana tumetoa tamko hili mapema kupitia wilaya zote kuwataka wanachama wetu kutoshiriki kwa namna yoyote ile,’’ alisema Bimani.

Alidai kuwa mkutano huo mkuu unaratibiwa kwa ajili ya kumuondoa Maalim Seif kwenye nafasi yake ya ukatibu mkuu.

Hata hivyo, naibu mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF Lipumba, Nassor Seif alisema kwa mujibu wa katiba ya chama chao mkutano mkuu huitishwa na baraza kuu la chama, hivyo iwapo baraza hilo litakaa na kuona ipo haja ya kuitishwa kwa mkutano huo basi hakuna wa kuzuia.

Seif alisema kwa mujibu wa katiba yao mkutano mkuu unaweza kufanyika kila mwaka kinyume na ilivyozoeleka sasa ndani ya chama hicho, hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Alisema mabadiliko ya muda wa mkutano huo hutokea kulingana na sababu za fedha.

“Acheni kuishi kwa ndoto kwani kila mmoja anafahamu ukweli uliopo hivi sasa kuhusu nani anafuata katiba ya chama na nani hafuati,” alisema Seif.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here