SHARE

Baadhi yetu tumekuwa tukiutumia mara kwa mara usemi wa kukataliwa kubaya au kukataliwa kunauma lakini si wote tunaofahamu kwa kina maumivu ya kukataliwa.

Ni ama tumesikia kwa marafiki zetu wa karibu waliokataliwa na tukatumia muda kuwafariji au kama tumekataliwa basi ni mara moja tu katika maisha yetu lakini wengine hata hawajawahi kukataliwa.

Mlemavu Jivunie Mbunda (35) kwake suala la kukataliwa limekwenda mbali kwani kabla ya ndoa yake ya hivi karibuni na Bahati Ramadhani, Mbunda amewahi kukataliwa mara 15 na wasichana tofauti tofauti.

“Nimewahi kuchumbia wanawake 15 kati yao, 10 walionyesha utayari wa kuolewa nami na watano nilikuwa nawajaribu lakini wote walinikataa kwa sababu ya ulemavu wangu,” anasema Mbunda.

Mbunda ana bahati ya kipekee kama lilivyo jina la mke wake Bahati kwani katika mazingira ya kawaida haikuwa rahisi kwake kupata mwanamke kutokana na umbile lake la ufupi.

“Kwanza kabla ya kuanza kuwatongoza wanawake, niseme sijui ulikuwa ni ushamba ama kutokujua tu, nikiambiwa na mwanamke kuwa, ananipenda na anataka niwe mume wake nilikuwa ninalia kwani niliamini anataka kuniua,”anasema Mbunda.

Mbunda anaeleza alijidharau na aliamini kutokana na ulemavu wake hakuna mwanamke ambaye angetokea kumpenda. Mwanamke aliyemwambia ‘nakupenda’ aliona kama anamkashifu hivyo aliumia moyoni.

“Nilivyokua na kujitambua, nilianza kujiona na mimi niko sawa na ninaweza kumpenda mwanamke na yeye akanipenda. Hapo ndipo nikaanza safari ya kumtafuta atakaye nipenda ili nimuoe.

“Kwa mara ya kwanza kabisa, kuna mwanamke nilitokea kumpenda, nikamfuata kwa ujasiri wote na kumweleza kwa lengo la kutaka kumuoa lakini aliishia kunitukana na kuniambia mimi kifupi nyundo atanipeleka wapi,” anasema Mbunda.

“Niliumia kwa kauli hiyo lakini sikufa moyo, niliendelea kumsaka mwanamke ambaye ningempenda na yeye akanipenda ili awe mke wangu lakini sikuweza kumpata nilishia kukashifiwa tu na wengine kunipiga kalenda wakionyesha wameshiba wakati hawajashiba.”

Mbunda anaeleza kuwa katika wanawake hao 10 aliowahi kuwatongoza akiwa na lengo la kuishi nao kama mke na mume walimweleza kuwa wana watu wao na hata alipowauliza wanaume walionao walishawahi hata kuwatolea barua ama kuwaeleza wazi kuwa wanataka kuwaoa, walimjibu, hapana.”

“Kila niliyekuwa nikimfuata ,utasikia anasema nina mtu wangu au subiri kwanza nitakujibu, inabaki subiri nina mtu wangu au subiri nitakujibu, mwisho wa siku wanakataa kwa kisingizio kuwa sina hadhi ya kuwa nao, nitawaaibisha,” anasema Mbunda.

Anasema mwaka 2007, alibahatika kumpata mwanamke ambaye alimtongoza na akakubalia kuwa mpenzi wake, wakaanza mahusiano na mwisho wa siku akampa mimba lakini alipogusia suala la kuoa mwanamke huyo akakataa.

“Mwaka 2016 mwanamke huyo aliniacha kabisa hata yale mahusiano ya kawaida alikataa na kuolewa na mwanaume mwingine. Nilikaa mpaka nilipokuja kumpata Bahati. Namshukuru Mungu kwa kunitunuku mke huyu, nampenda sana,” anasema Mbunda.

Kwa hali aliyonayo Mbunda hawezi kufanya jambo lolote bila ya kuwapo mtu wa karibu wa kumsaidia, ni lazima abebwe hata kama anahitaji kwenda katika mizunguko yak e yakutafuta riziki, bila hivyo mifuko yake haitaingiza kitu lakini Bahati amempenda hivyo hivyo.

Si mlemavu wa kwanza kuoa

Pamoja na misukosuko yote aliyopitia Mbunda ya kukataliwa hadi kumpata Bahati wake, bado yeye si mlemavu wa kwanza duniani kupenda.

Mwaka 2012 huko Arizona nchini Marekani, mwanadada mrembo, Mindie Kniss aliwashangaza wengi baada ya kukubali kuolewa na Sean Stephenson.

Mindie ana urefu wa futi 4 na sentimita 11 lakini mumewe Sean ana urefu wa futi mbili na inchi nane.

Utofauti wa mahusiano haya ni kwamba mwanaume (Sean) ni tajiri jambo ambalo linawafanya watu wengi wajenge hisia kwamba alichopenda Mindie kwa Sean ni pesa na si vinginevyo.

Hata hivyo hali ni tofauti kwa Bahati kwani mumewe Mbunda hana kitu, si tajiri badala yake anategemea pesa za misaada na ujasiriamali mdogo ambao pia haumwingizii pesa ya kutosha.

Mbunda na Bahati walifunga pingu za maisha 12 Mei mjini Liwale mkoa wa Lindi ikiwa ni miezi minne tangu wafahamiane kwa njia ya simu baada ya kuunganishwa na jirani yao.

Pamoja na ukweli kwamba ndoa ya Mbunda na Bahati imeendelea kuvuta hisia za wengi lakini kama ilivyo ada watu mbalimbali wameendelea kuidadisi ndoa hiyo kwa kujiuliza maswali mengi.

Miongoni mwa maswali hayo ni nini hasa kimemfanya Bahati akubali kuolewa na Mbunda? Je kuna kitu anatafuta? Pengine muda ni hakimu mzuri atakayekuja na jibu ya swali hilo.

Ripoti mbalimbali zikiwamo za mashirika ya Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa kundi hili la watu wenye ulemavu ndilo linaloathirika zaidi na matukio ya ukatili wa kijinsia na ukiukwaji haki za binadamu na kubaguliwa.

Asilimia 50 ya watu wenye ulemavu wakiwamo watoto hawapati huduma muhimu za kijamii, ikiwamo kuwa na mahusiano ya ndoa, afya na elimu.

Kwa mujibu wa Jarida la Child Protection lililotolewa na Shirika la Moja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), Tanzania linasema watoto wawili kati ya watano wenye ulemavu ndio wanaopata nafasi ya kwenda shule.

Pili Iyobhe mkazi wa Shatimba mkoani Shinyanga ni miongoni mwa kundi la walemavu ambao wamefikia umri wa kuoa ama kuolewa lakini bado hajapata mwenzi wa maisha na tatizo kubwa kwa mujibu wa Pili mwenyewe ni ulemavu wake.

Pili ni mlemavu wa viungo ana kimo kifupi kama Mbunda lakini yeye hawezi kukaa, ni mtu wa kulala tu na anatembea kwa kuvuta tumbo.

“Ninatamani kuolewa lakini sijabahatika kumpata mwanaume wa kunioa, unafikiri kuna mwanaume atakayenipenda mimi? Labda utokee muujiza kama uliompata mwenzetu Mbunda lakini si rahisi,” anasema Pili.

Wadogo wa Mbunda

Walemavu walio wengi wanaugulia maumivu ya upweke kama wanavyodai wadogo zake na Mbunda, Salama (22) na Bakiri (27) ambao wanasema kwamba wanaitamani sana ndoa, maisha ya upweke yamewachosha lakini ulemavu ni kikwazo kwao.

Salama na Bakiri ambao ni wadogo zake Mbunda wao ni walemavu wa viungo ambao kama alivyo kwa kaka yao Mbunda nao ni wafupi na kila wanachokifanya wanahitaji msaada.

Wadogo zake Mbunda nao tamaa yao kubwa ni kupata wapenzi kama ilivyo kwa kaka yao. “Natamani kuwa na mume na watoto, natamani sana, lakini sijabahatika kupata. Wanaume wananikataa sababu mimi ni mlemavu,” anasema Salama mdogo wake Mbunda.

Salama ambaye mara kadhaa alikuwa akilengwa na machozi wakati alipozungumza hasa alipogusia suala la yeye kuolewa na kupata watoto.

“Ninatamani kuwa na mtoto, hata kama nitakosa mume wa kunioa basi niwe na mtoto tu atakayenisaidia baadaye,” anasema Salama.

Salama anadai kwamba kwa sasa anaye rafiki wa kiume ambaye walikutana toka mwaka 2016 hata hivyo bado hana uhakika kama mwanaume huyo atamuoa.

“Ninaye rafiki wa kiume, anaonekana ananipenda lakini siwezi kuusemea moyo wake maana hajaonyesha dalili hata za kunichumbia,” anasema.

Salama anatamani kupata mume wa aina yoyote ambaye Mungu atamjalia.

Naye Bakiri kwa upande wake anadai kwamba anatafuta mke wa kuoa na anaomba Mungu amjaalie kama alivyomjaalia kaka yake.

“Suala la kaka yangu kuoa limenipa hamasa na imani yangu ni kwamba hata mimi ninaweza kuoa ama kumpata mke atakayenipenda,” anasema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here