SHARE

Mei 24 Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa jijini Mwanza kuzungumza na waandishi wa habari kupitia kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari nchini (UTPC).

Kiongozi huyo wa upinzani alipata fursa ya kumtembelea na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ofisini kwake ambapo viongozi hao walifanya mazungumzo ya dakika nane.

Mambo kadhaa yaliibuka wakati wa mazungumzo kati ya viongozi hao, kubwa ikiwa ni mipango na mikakati ya mkoa ya kiuchumi.

Akionekana mwenye bashasha, Maalim Seif akatumia fursa hiyo kumuuliza Mongella, nini kimefanyika na mikakati iliyopo ya kuinua uchumi wa wakazi na Mkoa wa Mwanza.

Mongella atiririka

Kutokana na swali hilo, Mkuu wa mkoa akampa mipango na mikakati ya kiuchumi ya mkoa wake katika kuongeza uzalishaji mali na mchango wa mkoa kwenye Pato la Taifa. Akasema Mwanza inatarajiwa kufikia zaidi ya Sh10 trilioni kutoka Sh7.4 trilioni za sasa ifikapo mwaka 2025.

“Maeneo ya kipaumbele kufanikisha lengo hilo ni sekta za ufugaji, uvuvi, utalii, uchimbaji na uchakataji wa madini, kilimo (cha umwagiliaji) na huduma za kijamii kama afya, elimu na michezo,” anasema Mongella na kuongeza:

“Pamba ni zao letu la kimkakati kwa ajili ya malighafi kwa viwanda vidogo, kati na vikubwa vilivyopo na vitakavyojengwa. Pia, tumeongeza na tutaongeza zaidi uzalishaji wa mpunga na alizeti kama mazao ya biashara na chakula,”

Akasema Mkoa wa Mwanza unaopakana na sehemu kubwa ya Ziwa Victoria pia imepanga kuboresha sekta ya uvuvi ambayo Mongella anasema imeanza kuimarika kwa idadi na ukubwa wa samaki kuongezeka baada ya Serikali kuendesha operesheni dhidi ya uvuvi na zana haramu ndani ya Ziwa Victoria.

“Uhakika wa upatikanaji samaki utawezesha kufufuliwa na kuviendesha kwa tija viwanda vya kuchakata mazao ya samaki ambavyo baadhi vimefungwa au kupunguza uzalishaji kwa kukosa malighafi,” anasema.

Dhahabu

Sekta ya madini, kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa ni miongoni mwa vipaumbele ambapo kiwango cha uzalishaji na uwekezaji kwenye viwanda vya kuchenjua dhahabu kitaongezeka kutokana na mazingira bora ya kibiashara inayowekwa na Serikali.

“Kuna viwanda zaidi ya 25 vya kuchenjua dhahabu kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa; sehemu ya dhahabu kutoka Chunya mkoani Mbeya pia huchenjuliwa Mwanza kwa sababu ya ubora wa teknolojia na ufanisi wa viwanda vyetu,” anatamba Mongella.

Uwekezaji

Vilevile mkuu wa mikoa akazungumzia mazingira bora ya uwekezaji na tija kwenye sekta za ufugaji inayolenga kuwezesha wafugaji kunenepesha mifugo kukidhi mahitaji na ushindani wa soko la ndani na nje ya nchi pamoja na ubora wa sekta ya utalii ni maeneo mengine ya kimkakati kwa mkoa wa Mwanza.

“Kupanuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kufikia kiwango cha Kimataifa kutawezesha ndege kubwa kutua Mwanza. Hii itaongeza idadi ya watalii kutokana na urahisi wa kufika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutokea Mwanza kulinganisha na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,” anasema.

Anasema mkoa huo pia una hifadhi ya Kisiwa cha Saanane ambayo ndiyo pekee nchini iliyoko katikati ya mji ikiwa na vivutio vya wanyama wakiwemo pundamilia, nyumbu, swala na aina mbalimbali za ndege, mawe marefu yaliyosimama peke yake na uvuvi wa kitalii.

Jiji la Mwanza, akasema pia ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki kutokana urahisi wa kwenda na kutoka Miji Mkuu ya Nairobi, Kenya, Kampala, Uganda, Kigali, Rwanda na Bujumbura nchini Burundi.

Kuondoa urasimu

Ili kufikia malengo tarajiwa, Mongella anasema mkoa wake utaunda timu ya pamoja ya Wataalam kutoka Mamlaka, Taasisi na idara za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali na leseni ili kuwapunguza urasimu wa kimfumo kwa wawekezaji wanaojitokeza kuwekeza mkoani humo.

“Hatulengi kuvunja sheria, kanuni na utaratibu; timu hii itakuwa na wajibu wa kuchukua uamuzi pale urasimu wa kimfumo unapokuwa kikwazo ya kufikia malengo yetu kiuchumi na kimaendeleo, hasa kwenye utoaji wa vibali na leseni za kuanzisha na kuendesha biashara,” anafafanua

Maelezo hayo yakaonekana kumkuna Maalim Seif ambaye alimwagia sifa Mongella na timu na akiwasisitizia kuhakikisha mipango hiyo inaleta tija na maendeleo ya haraka, kukuza na kuboresha uchumi wa wananchi, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Mwongozo wa uwekezaji

Novemba 27, 2017, Mkoa wa Mwanza ulizindua mwongozo wa uwekezaji ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa masuala ya kiuchumi na kijamii (ESRF), kwa ufadhili wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Kwa mujibu wa Mtaalamu kutoka ESRF, Dk Bohela Lunogelo, pato la mwananchi wa Mkoa wa Mwanza ni zaidi ya Sh2 milioni kwa mwaka.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here