SHARE

Kiwango duni kilichoonyeshwa na idadi kubwa ya ‘nyota’ wa kigeni katika michuano ya Ligi Luu Tanzania Bara, kimewaweka katika nafasi finyu ya kubaki kwenye klabu zao msimu ujao.

Hata hivyo, wapo baadhi ya mastaa wa kigeni waliziweka mgongoni timu zao na kuzisaidia kufanya vizuri baada ya kutoa mchango bora uliochangia mafanikio kwa klabu hizo.

Ingawa kulikuwa na zaidi ya wachezaji 30 wa kigeni ambao walisajiliwa kuzitumikia baadhi ya timu za Ligi Kuu, nyota zaidi ya 15 walionyesha kiwango bora ambacho kinaweza kuwabakiza na kukwepa panga katika dirisha kubwa la usajili.

Miongoni mwa wachezaji wa kigeni walioshindwa kukata kiu ya wadau wa soka ni Bernard Arthur, Michel Rusheshangoga, Laudit Mavugo, Youthe Rostand, Haruna Niyonzima, Enock Atta-Agyei, Juuko Murshid, Daniel Amoah, Yahaya Mohammed na Ivan Rugumandye.

Wengine ni Muroiwa Elisha, Nicholas Gyan, Marik Antil, Wisdom Mtasa Simbarashe Nhivi, Dan Usengimana, Joseph Owino, Uzoka Ugechukwu na Lubinda Mundia.

Wachezaji hao walionyesha kiwango cha kawaida kabisa na baadhi walijikuta wakisota benchi huku wakiendelea kuzitafuna klabu zao fungu kubwa la fedha zilizotumika kuwahudumia.

Mavugo aliyesajiliwa kwa mbwembwe na Simba mwanzoni mwa msimu wa 2016/2017 alishindwa kufua dafu mbele ya John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.

Benchi la ufundi la timu hiyo liliwapa nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na mchango wao katika kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.

Mshambuliaji Nicholas Gyan alishindwa kuhimili ushindani wa nafasi hadi kujikuta akihamishwa namba na kucheza beki wa kulia tofauti na mategemeo ya wengi kuwa angekuwa msaada kwa Simba katika kufunga mabao.

Kama kuna nyota wa kigeni walioboronga zaidi ni washambuliaji Yahaya Mohammed na Arthur wa Azam ambao walivunjiwa mikataba yao kwa nyakati tofauti kabla hata ligi haijamalizika kutokana na kiwango kibovu.

Alianza Yahaya Mohammed ambaye mkataba wake ulivunjwa wakati wa dirisha dogo la usajili, baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza mbele ya wazawa, Yahya Zayd, Shaaban Iddi na Mbaraka Yusuph na pengo lake lilizibwa na Arthur ambaye naye alitupiwa virago kabla hata ligi haijamalizika.

Timu iliyoonja shubiri ya kiwango kibovu cha wachezaji wa kigeni ni Singida United ambayo ndani ya msimu mmoja ilifanya usajili wa wachezaji 11 kutoka nje ya nchi na kulazimika kuvunja mikataba ya wengine ambao hawakumaliza hata msimu.

Mikataba ya Nhivi na Muroiwa ilivunjwa kabla ya ligi kumalizika wakati Mtasa alipelekwa kwa mkopo Stand United.

Usengimana licha ya kusajiliwa akiwa anaongoza kwa kufunga mabao nchini Rwanda, amepachika mabao yasiyozidi sita katika Ligi Kuu wakati Rusheshangonga, Antil, Mundia na Kambale Saritha walishindwa kuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho.

Kundi la wachezaji wa kigeni waliofanya vizuri wamo Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi wa Yanga, Emmanuel Okwi, James Kotei na Asante Kwasi (Simba), Blaise Bigirimana (Stand United), Yakubu Mohammed, Bruce Kangwa na Razack Abalora (Azam), Tafadzwa Kutinyu na Shaffiq Batambuze (Singida United).

Wakati Tshishimbi akiwa nguzo katika safu ya kiungo ya Yanga ambayo muda mrefu ilikuwa ikisuasua, alisaidia safu ya ushambuliaji kufunga mabao manne, Chirwa ndiye alikuwa mfungaji tegemeo wa timu hiyo msimu huu, akifunga mara 13.

Katika kikosi cha Simba, Okwi alichangia ubingwa akifunga mabao 20 wakati Kotei na Kwasi walikuwa muhimu katika safu ya ulinzi ambayo iliruhusu mabao 15.

Ndani ya kikosi cha Azam, nyota pekee wa kigeni walioonyesha kiwango bora walikuwa ni Kangwa, Abalora na Yakubu wanaocheza safu ya ulinzi ambao kiwango na umahiri wao katika kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani uliifanya timu hiyo kufungwa mabao machache zaidi sawa na Simba.

Wengine waliojitutumua na kuonyesha thamani zao Bigirimana, Kutinyu na Batambuze waliogeuka lulu kwa kuziimarisha safu za ushambuliaji na ulinzi katika kikosi cha Singida na Stand United.

Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, Juma Mgunda alisema usajili wa wachezaji wa kigeni hauzingatii ubora wa kiufundi.

“Sisemi wachezaji wa kigeni sio wazuri. Hapana ni wazuri lakini wanakuja huku wakiwa na viwango sawa na wachezaji wazawa hivyo wanajikuta hawana kipya wanachokiingiza kwenye timu,” alisema mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa Coastal Union.

Kocha msaidizi wa Njombe Mji, Mrage Kabange alisema kuwa kiwango duni cha wachezaji wageni kinasababishwa na mfumo wa usajili ambao umekuwa kichaka cha kusajili wachezaji wasiokuwa na uwezo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here