SHARE

Kitendo cha Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na mpinzani wake, Raila Odinga kuombana msamaha hadharani kimewavuta wanasiasa kupongeza na kutaka kiigwe, huku wengine wakisema ni vigumu kutekelezeka nchini kwa vile siasa za mataifa hayo mawili zinatofautiana.

Juzi, Rais Kenyatta aliungana na makamu wake, William Ruto kufanya maombi ya amani kwa taifa lao na kukutana na mpinzani wake, Odinga aliyeambatana na Kalonzo Musyoka ambao wote walisimama mbele ya hadhara kuombana radhi na kusameheana.

Wakizungumzia kitendo hicho baadhi ya wanasiasa nchini walisema jana kuwa viongozi hao wameonyesha uungwana kwa kukutana na kuzika tofauti zao, jambo ambalo linafaa kuigwa na viongozi wengine nchini na Afrika kwa ujumla.

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alikielezea kitendo hicho kuwa cha kijasiri na kuwa uchaguzi unapomalizika wananchi wanapaswa kupatana ili maisha yaendelee.

Alisema yale yaliyotokea Kenya yanaweza kufanyika pia hapa nchini iwapo pande zote zitakubaliana kufanya hivyo.

“Hapa kwetu Rais John Magufuli na mheshimiwa (Freeman )Mbowe (mwenyekiti wa Chadema) wanaweza kufanya hivyo. Mimi naona (Edward) Lowassa (waziri mkuu wa zamani) amefungua njia ya majadiliano kwa hatua yake ya kumtembelea Rais Ikulu. Pia nimefurahi kusikia kwamba Maalim Seif wakati alipomtembelea mkuu wa Mkoa wa Mwanza anasema yuko tayari kukutana na Rais, hatua hii ni mwelekeo chanya,” alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kugombea urais.

Alisema iwapo kuna chama kinaona kuna mambo wanataka Rais alegeze msimamo, waanze kujenga urafiki na chama tawala ili kuanzisha majadiliano, lakini siyo kutumia njia nyingine alizodai zenye kuleta utatanishi.

Hoja inayofanana na hiyo iliibuliwa pia na mwenyekiti wa UDP, John Cheyo aliyesema siku zote siasa siyo uadui na haiwezekani taifa kufanya uchaguzi likiwa katika hali ya uhasama na kuendelea nao hadi uchaguzi mwingine.

“Hili la Kenya ni mfano mzuri wa kuigwa na siku zote mimi nasisitiza kuwa siasa siyo uadui ila mnaweza kutofautiana katika mambo fulani, lakini siyo kujengeana chuki,” alisema

“Waamuzi wa mambo ya siasa ni wananchi, wakipiga kura wale walioshinda waendelee na kazi na wale walioshindwa wasubiri hadi uchaguzi ujao….siyo jambo nzuri kutengeneza uadui kati ya kiongozi A na kiongozi B.”

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema wanasiasa nchini wanapaswa kuiga yaliyofanywa na wenzao wa nchi jirani kwa lengo la kuleta maridhiano.

“Wapinzani wasichukuliwe kama maadui, wenzetu hapa nchini wanapaswa kuiga yale yaliyofanyika Kenya kwani Tanzania ni yetu sote na tujenge utamaduni wa kukosoana bila kutishana wala kutupwa magerezani,” alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kugombea ubunge Jimbo la Vunjo katika uchaguzi wa 2010.

Hata hivyo, alidai kuwa yale yaliyofanywa na wanasiasa wa Kenya si mageni nchini kwa kuwa yaliwahi kufanywa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na mpinzani wake Seif Sharrif Hamad walipokubali kuzika tofauti zao kwa ajili ya masilahi ya wananchi.

“Mwaka 2010 viongozi hao walishikana mikono na kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya kuendeleza Zanzibar, lakini leo hali hiyo haipo tena,” alisema.

Wakati wanasiasa hao wakitoa mwelekeo huo, kundi jingine la wanasiasa limechukulia tukio hilo kama jambo linalowafaa raia wa Kenya na haliwezi kukubalika katika siasa za Tanzania.

“Kwanza ni jambo la kufurahia kuona watu wakipatana maana kwenye vurugu hakuna maendeleo, lakini kusema sisi Tanzania tunaweza kujifunza nini kutokana na tukio hilo nadhani hakuna lolote la kujifunza kwa vile yale yaliyotokea Kenya hayapo hapa kwetu,” alisema Pius Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM.

Akifafanua zaidi, alisema hakuna jambo jipya lililofanywa na wanasiasa hao, bali wametimiza wajibu wa kiimani wa kusameheana na wamefanya mbele ya Mungu. “ Hilo walilolifanya ni jambo la kawaida tu tena lipo hata kwenye Biblia, mnapokosana tafuteni njia ya kusameheana,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe alipinga yale yaliyofanyika Kenya kufanywa hapa nchini akisema utamaduni wa Taifa hilo ni tofauti na ule wa Tanzania.

“Wenzetu wamestaarabika katika demokrasia, lakini sisi tunajikongoja tu. Sisi ni wajuaji wa kila kitu na tunaona hakuna haja ya kuombana msamaha. Siyo jambo rahisi kwa hilo kutokea nchini,” alisema Rungwe aliyekuwa miongoni mwa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.

Raila na salamu za JPM

Akizungumza jana kwenye maadhimisho ya miaka 55 ya Madaraka Day nchini Kenya, Raila Odinga alisema alipigiwa simu na Rais John Magufuli akimtaka amfikishie salamu zake kwa Rais Kenyatta na Wakenya kwa kuadhimisha siku hiyo.

“Kwanza nimeleta salamu kutoka kwa rafiki wa Wameru, Rais jirani wa Tanzania mheshimiwa Magufuli , wengine mnakumbuka nilimleta Magufuli hapa wakati tunazindua ujenzi wa barabara Meru, leo asubuhi amenipigia simu kwamba nikifika nilete salamu kwa Rais Uhuru,” alisema Odinga.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa alipoulizwa na Mwananchi alisema hana taarifa hizo.

“Mimi nashughulikia taarifa za kiofisi, sasa kama yeye ameongea na Rais kwa simu, muulizeni yeye, siwezi kuwa naangalia kila kitu anachofanya Rais na kutolea taarifa,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here