SHARE

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema wanaCCM watamkumbuka daima Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Abdurahman Kinana.

Kikwete amesema Kinana atakumbukwa kutokana na mchango wake mkubwa wa kukiimarisha chama hicho muda wote aliokaa kwenye nafasi hiyo.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Kikwete alimpongeza Kinana kwa kazi nzuri aliyokifanyia chama hicho na kumtakia mapumziko mema.

Kikwete alitumia ukurasa huo kwa kuandika: “Kwa heri Kinana. Hongera kwa kazi nzuri. Daima tutakukumbuka. Hongera Bashiru, nakutakia kila la heri. Hongera CCM, hongera Mwenyekiti Magufuli, Umoja ni Ushindi, Kidumu Chama Cha Mapinduzi.”

Licha ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Kinana alikuwa meneja wa kampeni za CCM tangu mwaka 1995 kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi hadi kuhakikisha CCM inaibuka na ushindi wa kishindo katika ubunge, urais na udiwani.

Mei 28, mwaka huu, Kinana alitangaza kung’atuka katika nafasi hiyo baada ya kudumu nayo kwa miaka sita tangu alipoteuliwa mwaka 2012.

Baada ya kuachia nafasi hiyo, Mwenyekiti wa CCM, John Magufuli, alimteua Dk. Bashiru kushika nafasi hiyo na kuthibitishwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.

Alhamisi ya wiki hii, katika hafla ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisi ndogo ya CCM, Lumumba, Kinana alisema amemkabidhi ofisi pamoja na kumtambulisha kwa watendaji na kumwonyesha kazi zilivyokuwa zikifanyika.

“Nimewaomba watendaji wakupe ushirikiano kama walivyofanya kwangu na waandishi nawaomba mpeni ushirikiano,” alisema Kinana.

Naye Dk. Bashiru alisema kazi aliyopewa si ya siasa za majukwani bali ni kazi ya mtendaji ikiwamo kubuni mikakati ya kutekeleza maazimio ya kikao.

“Kazi niliyopewa si siasa za majukwani, siasa za majukwani ni mwenyekiti wa chama akisaidiwa na makamu wake wawili, mikoani kuna wenyekiti wa vyama wa wilaya na mikoa, wabunge na madiwani,” alisema Dk. Bashiru.

Aliongezea kuwa:”Ni marufuku kwa watendaji kufanya kazi ya mwanasiasa. Kazi ya kupiga siasa safi ni wale waliochaguliwa kwa miaka mitano mitano. Watendaji tumeteuliwa naweza kukaa nusu saa au mwaka mmoja kwa hiyo kama mtendaji hamtaniona kwenye majukwaa kwa sababu wako waliopewa dhamana ya kukaa kwenye majukwaa,”.

Alisema kazi yake ni kubuni mikakati ya kutekeleza maadhimio ya kikao, kutoa taarifa zake, kusimamia maelekezo ya chama na kwamba masuala hayo sio ya kukaa jukwaani ni ya kukaa mezani.

Aidha, alisema kuwa jukumu alilokabidhiwa ni kwamba amekikuta chama kimeshaanza utekelezaji wa ilani na kwamba yeye atakwenda kuanzia alipokikuta.

“Kwa mfano mwaka 1992 wakati tunaanza mfumo wa vyama vingi na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, Chama cha Mapinduzi kiliahidi kufanya utaratibu wa haraka ili kuhamia mkoani Dodoma. ukisoma ilani hilo utaliona,” alisema.

”Mwaka 1995 hatukuweza mwaka 2000, 2005, 2010 hatukuweza lakini 2015 tumeanza. Hicho ni kipaumbele cha utekelezaji tunazozitoa hata zile ambazo zinakuwa ziko nyuma. , nasikia kuna wengine wanasema kuhamia Dodoma haikuwa kwenye ilani someni vizuri ilani mtaona tumelipanga tangu mwaka 1995,” alisema

Dk. Bashiru alisema jukumu lake ni kutekeleza ilani ya chama na vipaumbele hivyo vipo kwenye ilani ambayo imewapa ridhaa ya kuongoza serikali zote mbili.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here