SHARE

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewapongeza mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kwa kuingia fainali ya michuano ya Sportpesa inayofanyika Kenya.

Dk Mwakyembe ametoa pongeza hizo leo Ijumaa Juni 8, 2018 bungeni mjini Dodoma kabla ya kujibu maswali mbalimbali ya wabunge yaliyoelezekwa kwa wizara yake.

“Ninawapongeza mabigwa wa Bara kutinga fainali ya Sportpesa, Simba wamethibitisha kuwa walipata ubingwa huo si kwa kubahatisha bali kwa soka la viwango na sasa wanaingia fainali kupambana na mabingwa wa Kenya,”amesema.

Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mussa Sima amehoji kuhusu zawadi inayotolewa kwa mabingwa kwamba haiendani na gharama ambazo timu hutumia kusajili, kutaka kujua mpango wa Serikali kuboresha eneo la zawadi.

Akijibu swali hilo, Dk Mwakyembe amesema, “sisi kama wizara hatujaona tatizo la usajili na ushindani na kama ni matumizi ya pesa, soka la sasa ni pesa kama huna pesa huwezi. Unaweza kuona timu kama Singida inavyofanya vyema na tuwaombee waweze kuwa washindi wa tatu katika michuano ya Sportpesa.”

Katika swali lililoulizwa na mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu alitaka maelezo ya Serikali kama ina mpango wa kuboresha eneo la VIP la Uwanja wa Taifa kwa maelezo kuwa eneo hilo halina zuio la watazamaji mpira, iwapo mvua itanyesha.

“Ni kweli kuna upungufu katika uwanja wetu wa Taifa na ndio maana tulipokuja kuomba tutengewe fedha za ukarabati wa uwanja mlikubali. Kiasi cha Sh1 bilioni kilichotengwa kitakwenda kufanyia mabadiliko na katika siku za usoni mtarajie kuona marekebisho hayo.”


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here