SHARE

KIUNGO mshambuliaji wa Singida United, Deus Kaseke anatarajia kuondoka nchini na kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kusaini mkataba mpya na timu moja ya huko, imeelezwa.

Mbali na Kaseke, pia kiungo, Mudathir Yahya, hatakuwapo kwenye kikosi hicho katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mudathir anarejea Azam FC ambayo msimu ujao itakuwa na kocha mpya, Hans van der Pluijm ambaye amechukua mikoba ya Mromania, Aristica Cioaba.

Akizungumza na gazeti na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alisema kuwa wamempa ruhusa Kaseke aweze akasaini mkataba na timu yake mpya huku akimtaja Mudathir amewaeleza anarejea Azam FC ya jijini Dar es Salaam.

“Hatutakuwa na Kaseke katika msimu ujao, amepata timu nyingine ya kuichezea Afrika Kusini, hivyo hatokuwa sehemu ya kikosi chetu, pia Danny Usengimana anaenda Rwanda,” alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, Sanga hakuwa tayari kuweka wazi jina la timu ambayo Kaseke anatarajia kujiunga nayo baada ya kumalizika kwa mashindano ya SportPesa Super Cup huko Kenya.

Tayari Azam FC ilishatangaza kumsajili mshambuliaji wa Singida United, Tafadzwa Kutinyu ambaye msimu uliopita, aliisaidia timu hiyo kufanya vizuri na hatimaye kucheza fainali ya Kombe la FA kwa mara ya kwanza.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here