SHARE

MSHAMBULIAJI mpya wa Azam FC, Donald Ngoma atakuwa nje kwa muda wa miezi miwili na nusu kwa ajili ya kupata matibabu ya kuuguza mguu wake alioumia akiwa Yanga.

Taarifa iliyopatikana jana kutoka Azam FC baada ya kumpeleka Afrika Kusini mshambuliaji huyo inasema kuwa baada ya kumaliza uchunguzi, alipatiwa matibabu na amepewa programu maalum ya mazoezi ambayo ataifanya chini ya usimamizi wa daktari wa klabu yake mpya.

Chanzo chetu kinasema kuwa baada ya Azam FC kubaini tatizo la Ngoma si kubwa, imeamua itampatia mkataba rasmi ili aweze kuitumikia timu yao baada ya kupona.

“Taarifa za vipimo za Ngoma ambaye aliambatana na daktari wa timu (Mwanandi Mwankemwa) huko Afrika Kusini zinasema atakaa nje kwa muda wa miezi miwili na nusu, Azam FC imeridhika kumsajili Ngoma,” kilisema chanzo chetu.

Ngoma na Mwankemwa walitarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam jana usiku na leo ndiyo atasaini mkataba wa kujiunga rasmi na Azam FC.

Baada ya kusaini, Ngoma atarejea kwao Zimbabwe kwa mapumziko ya wiki tatu kabla ya kurejea nchini kuanza maandalizi ya msimu mpya akiwa na wachezaji wenzake wa timu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Kombe la Kagame.

Wakati huo huo, Azam FC iko katika mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji Ditram Nchimbi kutoka Njombe Mji FC ambayo imeshuka daraja.

Endapo Azam FC itafanikiwa kumnasa mshambuliaji huyo, atakuwa ni mchezaji wa tatu kusajiliwa baada ya Ngoma na Mzimbabwe mwingine, kiungo Tafadzwa Kutinyu aliyetua akitokea Singida United ya mkoani Singida huku pia imeshamtangaza kocha wa zamani wa Yanga, Hans van van der Pluijm, atakuwa na kikosi hicho katika msimu ujao.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here