SHARE

Sakata la amri ya kuwakamata na kuwafunga jela wakurugenzi wa Tip Top Connection Company Limited, Hamis Taletale na ndugu yake Idd Shaban Taletale, limechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhoji uhalali wa amri hiyo.

Amri ya kuwakamata na kuwafunga jela Taletale, maarufu kama Babu Tale na ndugu yake ilitolewa na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri, Februari 16 akielekeza kuwa wapelekwe katika gereza la Ukonga na April 4, 2018, akatoa hati ya kuwakamata.

Naibu Msajili Mashauri alitoa amri na hati hiyo baada ya Babu Tale na nduguye kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama hiyo, iliyomwamuru kumlipa fidia ya Sh250 milioni Mhadhiri wa Dini ya Kiislam, Sheikh Hashim Mbonde, katika kesi ya ukiukwaji wa hakimiliki.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo juzi, Jaji Edson Mkasimongwa alihoji uhalali wa amri hiyo na kuwataka mawakili wa pande zote waieleze Mahakama iwapo msajili wa Mahakama ana mamlaka kisheria kutoa na kusaini amri ya kumkamata na kumfunga mtu jela.

“Katika shauri hili nimejifunza kwamba naibu msajili alitoa amri washindwa tuzo wakamatwe na kupelekwa jela kama wafungwa wa madai. Mshindwa tuzo alikamatwa akaletwa mbele ya msajili lakini msajili aliyetoa amri hiyo hakuwepo.

“Lakini naibu msajili aliyetoa amri hakuwapo ili aidhinishe kupelekwa jela, aliyekuwapo akaona shaka ndipo suala likaja kwangu kama Kaimu Jaji Mfawidhi. Hivyo nikajiuliza maswali, kama amri hiyo ilikuwa sahihi,” alisema Jaji Mkasimongwa.

Jaji Mkasimongwa alifafanua kuwa haimaanishi kwamba kilichofanyika kwa msajili kusikiliza maombi ya utekelezaji wa hukumu si sahihi kwani hilo liko kwenye mamlaka yake, lakini akasema anachotaka kujua ni kama msajili ana mamlaka ya kutoa amri ya mtu kukamatwa na kufungwa jela


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here