SHARE

Mwanafunzi mwenye ulemavu Zawadi Msigala ndiye anayeishi kwenye nyumba waliyokuwa wanaishi pacha walioungana marehemu Maria na Consolata, Kilolo mkoani Iringa.

Mwanafunzi huyo alichukuliwa na Shirika la Maria Consolata baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na ulemavu wake.

Awali, baada ya Zawadi kuhitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Tanangozi, alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Wavulana ya Songea lakini hakuweza.

Katika msiba wa Maria na Conslata, Zawadi alionekana akiwa mwenye sura ya huzuni juu ya baiskeli yake ya miguu mitatu pembeni mwa jeneza la pacha hao.

Maria na Consolata walifariki dunia Juni 2 katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa.

Mkuu wa Shirika la Maria Consolata, Jane Nugi alisema juzi kwamba tayari wameanza kumlea Zawadi kama ilivyokuwa kwa Maria na Consolata na wanatamani kuona ndoto zake zinatimia.

Alisema Zawadi ameanza masomo ya sekondari katika shule ya Maria Consolata ‘Nyota Ndogo’ waliyosoma Maria na Consolata kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Zawadi tupo naye na anaishi kwenye ile nyumba waliyokuwa wanaishi Maria na Consolata anaendelea vizuri na tunaangalia namna ya kumsaidia zaidi aendane na kasi ya wenzake,” alisema na kuongeza:

“Kama tulivyokuwa tunawapenda watoto wetu, Maria na Consolata ndivyo tunavyompenda Zawadi, natamani kuona anatimiza ndoto zake kimaisha,” alisema.

Alisema tofauti ya pacha hao na Zawadi ni namna wanavyoandika na kupokea mambo.

“Zawadi anaandika kwa kompyuta na anatumia miguu lakini kina Maria na Consolata walikuwa wanaandika kwa mikono. Pia Zawadi anajifunza polepole kwa hiyo anahitaji uangalizi wa hali ya juu wakati Maria na Consolata walikuwa wanaenda sawa na wanafunzi wengine,” alisema.

Katika mahojiano, Zawadi aliyekuwa akisaidiwa na kituo cha walemavu cha Nyumba Ali alisema amefanikiwa kuandika kitabu kwa kutumia miguu akielezea changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu.

Ndoto yake nyingine ni kuonana na Rais John Magufuli akisema akibahatika, atamuomba atoe kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu rafiki ya watu wenye ulemavu hasa shuleni.

“Natamani kusoma kwa bidii nije kuwa mwanasheria, pia natamani kuona siku moja Tanzania inaongozwa na watu wenye ulemavu,” alisema.

Kilicho mkutanisha Zawadi na shirika hilo ni uwezo wake mkubwa kiakili.

Mlezi wake wa awali katika kituo cha Nyumba Ali, alisema tangu akiwa darasa la kwanza, mlemavu huyo anayeandika kwa miguu kwa kutumia kompyuta, alikuwa akishika nafasi ya kwanza hadi ya tatu darasani.

“Tunaamini atafika mbali zaidi ya alipo kutokana na uwezo wake mkubwa darasani,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here