SHARE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba amesema wizara hiyo imeunda kamati maalumu kuchunguza sababu za kujengwa kwa kituo cha mradi wa mabasi yaendayo haraka katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam.

Hivi karibuni kituo hicho kilifungwa baada ya kukumbwa na mafuriko kutokana na mvua za masika zilizosababisha pia Barabara ya Morogoro kufungwa katika eneo hilo.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni, meneja wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Amos Gellert alisema walilazimika kuhamishia ofisi katika kituo cha Gerezani na kutumia moja ya mabasi kama ofisi, huku akisema mafuriko hayo yamesababisha hasara ya asilimia 30 ya mapato ya mradi huo kwa mwezi.

“Kuna kamati maalumu zimeundwa kuchunguza jambo hilo ili kulitafutia ufumbuzi. Zitakapokamilisha kazi ndiyo zitatushauri,” alisema Makamba bila kufafanua kamati hizo zitamaliza lini kazi.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Clouds wiki iliyopita Waziri Makamba alikaririwa akisema taratibu za mazingira hazikuzingatiwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

“Ni kweli kwamba Nemc (Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira) walifanya tathmini ya athari za mazingira katika eneo lakini nyaraka zinaonyesha watekelezaji wa mradi hawakufuata masharti ya mamlaka hiyo,” alisema Makamba.

Nemc ilivyotoa kibali cha ujenzi

Mkurugenzi wa Tathmini ya Mazingira wa Nemc, Dk Fadhila Khatib alisema mradi huo ulijengwa baada ya kukosa eneo jingine la kutumia.

“Eneo la mradi la Jangwani lilikubaliwa kutumiwa kwa ajili ya mradi baada ya kukosa eneo jingine la wazi ili kuruhusu mradi uanze kutekelezwa. Wizara ya Ardhi ilitoa asilimia 10 ya eneo la Jangwani kwa Dart ili kujenga kituo (depot),” alisema Dk Fadhila na kuongeza:

“Eneo la Jangwani kwa asili ni eneo la mafuriko hasa wakati wa mvua kubwa. Ili kujenga kituo katika eneo hilo tathmini ilifanyika na kuainisha mambo mbalimbali yaliyohitaji kufanyiwa kazi ili kuruhusu mradi kutekelezwa.”

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Maji (hydrological study) ili kuanisha changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.

“Ujenzi wa depot uzingatie kujaza udongo na kuinua eneo la mradi ili liwe juu kuliko eneo linalozunguka. Kupanua daraja la Mto Msimbazi eneo la Jangwani ili kuwezesha maji kupita kirahisi, kuongeza makaravati (box culverts) katika eneo hilo ili kuongeza njia ya maji kupita kirahisi,” alisema.

“Kusafisha mto kwa kuondoa mchanga na takataka zinazoletwa na maji ili kuhakikisha kina cha mto kinabaki kuruhusu maji kupita,” aliongeza.

Hata hivyo, alisema pamoja na mradi huo kutekeleza masuala ya kitaalamu, wakati wa ujenzi bado changamoto ya mafuriko katika kituo imeendelea kuwapo.

“Kinachochagiza tatizo hili ni takataka na mchanga unaozolewa na maji kutoka vyanzo vya mto kukwama kwenye daraja hivyo kupunguza kina cha mto. Hali hiyo husababisha maji kupita taratibu hivyo kutuamisha mchanga na kuzuia mtiririko mzuri wa maji,” alisema Dk Fadhila.

Hata hivyo, meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alipoulizwa kwa simu kuhusu masharti ya Nemc hasa upanuzi wa madaraja katika Barabara ya Morogoro alisema hakukuwa na maelekezo kama hayo.

“Hakuna maelekezo tuliyopewa na Nemc. Sisi tulizingatia utaalamu. Wao wana majukumu yao na sisi tuna majukumu yetu. Wapo watu wa jamii wanaohusika na makazi, takataka, wapo watu wa maji, kila mtu na majukumu yake. Ukiharibu kimoja umeharibu vyote,” alisema Ndyamukama.

Sheria zilivunjwa?

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa maofisa wa Nemc alisema mradi huo haukuzingatia kikamilifu baadhi ya sheria.

Alisema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 kifungu cha Kifungu cha 57 (1) hakikuzingatiwa. Kifungu hicho kinakataza shughuli za binadamu katika maeneo oevu.

“Kwa kuzingatia kifungu cha (2), ndani ya mita 60 hakutafanyika shughuli yoyote ya binadamu ya kudumu au ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira au utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa, au miambao ya asili ya ziwa,” alisema.

Hata hivyo, kifungu cha (2) kinampa mamlaka Waziri anayehusika na mazingira kuweka miongozo ya kuendesha shughuli za binadamu ndani ya maeneo yaliyoelezwa kwa mujibu wa kifungu cha 1.

Ofisa huyo pia alitaja Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya 2007, kifungu cha 25 na Sheria ya Ardhi Na.5 ya 1999 kifungu cha 7 (a-d) ambazo zinataka maeneo oevu yalindwe.

Kuhusu hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Vedasto Makota alisema Sheria ya Mazingira iliyotungwa baada ya Sheria za Ardhi na Mipango Miji ina nguvu zaidi.

“Unajua watu hawaelewi kuhusu Sheria ya Udhibiti wa Mazingira. Sheria hiyo imekuta Sheria ya Ardhi na hiyo ya Mipango Miji zikiwa zimeshatungwa, kwa hiyo inatumika kunapokuwa na mvutano wa sheria nyingine,” alisema Dk Makota.

Pamoja na hayo, Dk Makota alisema kwa sasa siyo muda wa kuzungumzia utata wa sheria hizo, bali kuangalia suluhisho la kuboresha bonde hilo.

“Jambo la msingi kwa sasa ni kuangalia mipango iliyopo ya kudhibiti bonde hilo. Kuna mabadiliko ya tabianchi, mvua zimenyesha sana na mafuriko yametokea. Wasiliana na Manispaa ya Kinondoni wakupe mpango wa kudhibiti bonde hilo. Tuachane na hizi sheria, tuangalie tunatokaje hapo tulipofikia,” alisema Dk Makota.

Mkurugenzi wa Chama cha Watetezi wa Mazingira (Leat), Dk Lugelemeza Nshala alisema licha ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kumpa mamlaka waziri kutumia maeneo hatarishi, bado anatakiwa kufuata ushauri wa Nemc.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here