SHARE

SERIKALI imepiga marufuku waajiri kuwataka wastaafu wafuatilie nyaraka za malipo ya pensheni kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii huku ikisisitiza kuwa kuanzia sasa haitamvumilia mwajiri yeyote atakachelewesha mafao kwa wastaafu.

Imesema jukumu hilo la kufuatilia mafao ya wastaafu linapaswa kufanywa na maofisa utumishi na endapo watashindwa kufanya hivyo watawajibishwa.

Serikali imetoa kauli hiyo kutokana na kile ilichokiri kuwapo kwa ucheleweshaji wa mafao kutokana na baadhi ya maofisa utumishi kushindwa kushughulikia nyaraka muhimu za wastaafu zinazohitajika katika ulipaji wa mafao hayo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Kapteni (mstaafu) Geogre Mkuchika, ndiye alitoa kauli hiyo ya serikali alipozungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari na Elimu ya Bunge, jijini Dodoma jana.

Mkuchika alisema kumekuwapo na changamoto ya wastaafu kutolipwa mafao kwa wakati pindi wanapostaafu huku wengine wakipoteza maisha kabla ya kupata mafao yao, ilhali sheria na taratibu zinataka mtumishi alipwe mafao yake ndani ya siku 60 baada ya kustaafu.

Alisema baadhi ya waajiri wamekuwa kikwazo katika upatikanaji wa mafao kutokana na kutowasaidia watumishi wao kukamilisha nyaraka muhimu pindi wanapostaafu.

Waziri Mkuchika alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwaondolea kadhia wastaafu kufuatilia mafao yao.

“Kuanzia leo (jana) ni marufuku kwa ofisa au mwajiri kumtaka mstaafu kufuatilia mafao yake kwenye mifuko au wizarani. Kama kuna nyaraka za kupeleka wizarani au katika mfuko, hilo ni jukumu la maofisa utumishi na si wastaafu,” alisema.

“Ofisa utumishi atakayezembea atawajibishwa. Kila mwajiri ahakikishe taarifa za watumishi zinakusanywa, kuhakikiwa, kuhuishwa na kuweka utaratibu kushughulikia watumishi wanaokaribia kustaafu kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.”

Waziri huyo pia alibainisha kuwa licha ya serikali kutoa maelekezo ya kuweka taarifa za watumishi kwa nyakati mbalimbali, bado mfumo huo umeendelea kuwa na taarifa za watumishi zisizokuwa sahihi.

Mkuchika aliwataka waajiri kusimamia na kuhakikisha kila mtumishi anakuwa na taarifa sahihi za majina, cheo, umri na elimu ili mwaka mpya wa fedha utakapoanza siku 22 zijazo, kila mtumishi awe na taarifa sahihi.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here