SHARE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wasikubali kuchonganishwa.

Alisema Serikali haiongozwi kwa misingi ya kidini bali imeziachia taasisi za kidini zifanye kazi kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi na malengo yaliyokusudiwa katika uanzishwaji wake.

Majaliwa alisema hayo juzi alipozungumza na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza baada ya futari aliyowaandalia. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na waumini wa madhehebu mbalimbali.

Waziri mkuu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, jambo litakalowawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu.

“Nawaasa viongozi wa dini msikubali kutumia makundi mengine nje ya taasisi zenu kwa ajili ya kuwazungumzia masuala yenu kwa sababu watawachonganisha na Serikali ambayo haipo kwa ajili ya kugombana na taasisi yoyote,” inasema taarifa ya ofisi ya waziri mkuu ikimkariri Majaliwa.

Awali, mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella alimshukuru waziri mkuu kwa ukarimu wake kwa kuwaalika wakazi wa Mwanza katika futari hiyo.

“Mwanza tumejipanga na tunashirikiana na taasisi kwenye nyanja zote, tupo pamoja na tunashirikiana katika kuimarisha amani na utulivu,” alisema Mongella.

Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Amani ya mkoa wa Mwanza, Charles Sekelwa alisema wanaiunga mkono Serikali katika kudumisha amani na wataendelea kushirikiana nayo.

Sekelwa ambaye ni Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), alisema awali kulikuwa na changamoto ya matabaka ya kidini iliyosababisha kutoelewana baina ya Waislamu na Wakristo, lakini kamati yao ilifanya kazi yake na sasa hali ni shwari.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here