SHARE

SERIKALI ya Saudi Arabia imesema itagharamia matibabu nchini humo kutenganisha pacha walioungana, Anisia na Almesia, wenye umri wa miezi mitano, yatakayofanyika nchini Saudi Arabia.

Watoto hao walizaliwa Januari 29, wilayani Misenyi katika Kituo cha Masista cha St. Theresa Omukajunguti Kata ya Kyaka na kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam mapema mwezi Februari, ambako wamewekwa kwenye wodi maalumu ya jengo la watoto ya Magufuli, wakipatiwa matibabu ya awali kabla ya kupelekwa Saudia Arabia kwa matibabu.

Watoto hao wa Jonisia wameungana eneo kubwa la kifua na tumbo, lakini kila mmoja ana mfumo wake wa hewa.

Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al – Hazani alilieleza gazeti la HabariLeo jana kuwa watoto hao watafanyiwa upasuaji huo wa kuwatenganisha katika Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical iliyopo Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, ambako kuna madaktari bingwa wa upasuaji.

Alisema mpango huo wa kufanikisha matibabu ya upasuaji wa kuwatenganisha mapacha hao, unafanywa kwa ushirikiano wa ubalozi wa Saudi Arabia nchini chini ya balozi wake Mohamed Bin Mansour, uongozi wa Hospitali ya Muhimbili na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga.

“Mara tu mipango na maandalizi itakapokamilika, tunatarajia watoto kuondoka kwenda Riyadh mwishoni mwa mwezi huu,” alisema Al-Hazani.

Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical huko Riyadh, ina uwezo mkubwa ikiwa na vifaa vya kisasa na vitanda 1,501 na ilianza shughuli zake Mei 1983.

Tangu wakati huo, imeendelea kupanuka, huku ikitoa huduma kwa idadi ya wagonjwa wanaokua kwa kasi katika maeneo yote.

Mama wa pacha hao, Jonisia Jovitus (21) alisema tayari watoto wake wamechukuliwa vipimo mbalimbali na jopo la madaktari wa Hospitali ya Muhimbili na kuvituma Saudi Arabia.

Akizungumza na gazeti la HabariLeo, mama wa mapacha hao alisema “madaktari wameniambia walishatuma vipimo Saudi Arabia na uwezekano wa watoto wangu kutenganishwa upo, naomba Mungu asaidie hili lifanikiwe… ila walichoniambia ni kuwa wanangu wakifanikiwa kutenganishwa salama watakuwa walemavu, mmoja atakuwa na mguu mmoja na mwingine ana miguu miwili, lakini huo mmoja hauna nguvu umepooza. Ninachoomba kwa sasa ni kuwaona watoto wangu wametenganishwa na kuwa salama, naomba jamii iniombee ili lifanikiwe.”

Uongozi wa Hospitali wa Muhimbili kupitia kwa Ofisa Uhusiano, Aminiel Eligaesha ulisema kuwa utaweka wazi kuhusu mchakato mzima wa watoto hao madaktari watakapokuwa tayari.

Awali, uongozi huo wa Muhimbili ulikuwa uzungumze na vyombo vya habari juzi, lakini waliahirisha kwa kile kilichoelezwa kuwa wahusika wamepata dharura, hivyo vyombo vya habari vitaarifiwa siku itakayoitishwa upya mkutano huo.

HabariLeo imezungumza na madaktari mbalimbali, kujua hasa chanzo kinachosababisha kuungana kwa pacha. Sababu za kuzaliwa wakiwa wameungana Dk Zaituni Bokhari, daktari bingwa wa upasuaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alisema kuwa hadi sasa hakuna sababu maalumu inayojulikana kisayansi.

Aliongeza kuwa pacha walioungana huwa ni matokeo ya kushindwa kukamilika kwa mchakato wa yai kugawanyika na hatimaye kila upande uanze kujenga viungo vyake ili wapatikane pacha wanaofanana.

Mchakato huu hutakiwa kufanyika kati ya wiki ya tano na wiki ya nane ya ujauzito.

Hata hivyo, kwa sababu ambazo bado hazijajulikana, mchakato huo hugoma kukamilika katika kipindi hicho na kusababisha kuzaliwa kwa pacha walioungana.

Alisema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kuna vihatarishi, vinavyoweza kusababisha yai lishindwe kutengana sehemu mbili, kama inavyotakiwa na kutaja sababu hizo hatarishi kwa wazazi wote wawili kunywa pombe kupindukia, kuvuta sigara kupita kiasi, mtindo wa vyakula visivyofaa kama mafuta mengi, unene kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

“Tunadhani vihatarishi hivi vinaweza kusababisha mtu kuzaa mtoto asiye na afya au pacha walioungana, nashauri pia mama kuanza kutumia madini ya folic acid pale ambapo anajitayarisha kubeba mimba,” alisema.

Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa, tafiti zinaonesha kuwa tatizo la watoto pacha kuzaliwa wakiwa wameungana ni mara chache kutokea duniani ambapo kati ya kila watoto 100,000 wanaozaliwa, ni tukio moja huwa ni la pacha walioungana.

Pia, wingi wa kuungana huku hutofautiana ambapo pacha walioungana tumboni ndio wanaoongoza kuzaliwa kwa asilimia 47; uti wa mgongo (asilimia 26); na pacha wanaozaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kichwa ni asilimia mbili. Mapacha wanazaliwa huku mmoja akiwa hajakamilika viungo vyake au Conjoined Tetrapus Parasyticus Twins ni nadra zaidi kutokea.

Daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Mwananyamala, Fabia Tumai alisema hakuna sababu yoyote maalumu inayosababisha watoto kuungana tumboni, ni namna tu jinsi wanavyokaa katika mji wa uzazi, haina tofauti na ndizi pacha. Mimba inatungwaje?

Akifafanua hatua ya utungwaji mimba mpaka kuzaliwa pacha, Dk Fabia alisema “Kipindi cha ovulation ndipo ambapo mwanamke anaweza kushika mimba. Ovulation ni kipindi ambacho yai kubwa ama yai lililo tayari hutoka kuelekea kwenye tumbo la uzazi kupitia mirija ya ovari.

“Yai hilo kwa bahati nzuri likikutana na mbegu ya kiume hurutubishwa katika kipindi cha saa 24 (baada ya muda huo yai hupoteza uwezo wake). Iwapo yai litarutubishwa ndani ya muda huo na kisha kujikita katika mfuko wa uzazi basi mimba itakuwa imetungwa. Iwapo yai halikurutubishwa hutolewa nje kama damu ya hedhi.

Mapacha hutokeaje?

“Hapa tukumbuke kuwa kuna pacha wa aina mbili, mapacha wanaofanana (Identical twins) na pacha wasiofanana (Fraternal twins). Mapacha wasiofanana hutokea pale mwanamke anapotoa mayai mawili kuelekea kwenye tumbo la uzazi. Hii ina maana ni mwanamke ama mwili wa mwanamke unaosababisha mayai mawili kuachiliwa kwa pamoja.

“Baada ya hapo mayai haya hukutana na mbegu za kiume yenye nguvu ambapo hurutubishwa ndani ya muda maalumu na kisha hujikita kwenye mfuko wa uzazi, hivyo basi hata kama mwanaume angetoa mbegu milioni moja lakini yai la mwanamke likitoka moja basi mtoto atakayepatikana atakuwa ni mmoja tu.

“Huo ni upande wa pacha wasiofanana (Fraternal twins). Kwa upande wa mapacha wanaofanana (Identical twins), hadithi ni tofauti kidogo, baada ya yai kurutubishwa na mbegu ya kiume na kujikita kwenye mfuko wa uzazi kwa sababu zisizofahamika kisayansi huamua kujigawa na kutengeneza watoto pacha. Pacha hawa kwa kawaida hufanana sana na huwa ni wa jinsia moja tofauti na ‘fraternal twins’ ambao huweza kuwa wa jinsia mbili tofauti ama jinsia moja.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here