SHARE

NYUMBA 85 na zaidi ya magari ya 10 ya wakopaji katika benki nne nchini, zimewekwa katika mnada wa hadhara, baada ya wakopaji kushindwa kurejesha mikopo waliochukua kwa dhamana ya mali hizo.

Kwa mujibu wa matangazo ya kampuni za udalali ndani ya siku 57 tangu Aprili 20, mwaka huu na kampuni zilizopewa kazi ya kuendesha mnada kwa niaba ya benki hizo, wakopaji hao walipewa muda wa siku saba kulipa madeni yao kabla ya mali zao kuuzwa kwa mnada.

Katika tangazo la Aprili 20, nyumba 43 ziliwekwa kwenye mnada huku tangazo la Mei 23 likiweka nyumba 21 na magari sita.

Aidha, tangazo la juzi, nyumba 20 na magari manne yalitangazwa huku wakopaji wakipewa siku saba hadi Juni 14 na 21, mwaka huu, kumaliza kulipa madeni yao vinginevyo mali hizo zitauzwa.

Tangazo lililotolewa juzi kwenye moja ya gazeti la kila siku, kampuni za udalali za Koti, Kiboko, Waungwana, Nkya, Jagro, Tanzania na Nolic, kwa niaba ya Benki ya Access Limited, walitangaza kuuza kwa mnada nyumba, magari, vifaa mbalimbali na viwanja.“Mali hizi ziliwekwa kama dhamana ya mikopo na wateja wa benki wameshindwa kulipa kwa mujibu wa mkataba husika. Ifahamike zitakapopita siku 14 kwa dhamana ya nyumba au kiwanja na siku saba kwa vifaa vingine na magari tangu kutoka gazeti hili, mali hizi zitauzwa” ilifafanuliwa kwenye tangazo hilo.

Aidha, tangazo hilo lilifafanua kuwa dhamana husika (mali) zitauzwa kwa njia ya mnada husika siku iliyopangwa ambao utafanyika sehemu mali zilipo.

Tangazo hilo limeeleza kuwa nyumba hizo ziko maeneo ya Yombo, Mtoni Kijichi, Mtongani, Kimara Temboni, Msasani, Temeke Kiboko, Tabata, Mbagala, Kinzudi kwa Mtenga, Kigamboni, Mbezi, Gongo la Mboto, Chamazi jijini Dar es Salaam, Tabora, Kahama na Mbeya mjini.

Katika tangazo la Aprili, Benki ya EFC ilitangaza mnada wa nyumba 43. Katika hizo, wateja 24 kati yao, walikopa kati ya Sh. milioni 30 na 343, huku wakopaji 19 wakiwa wenye mikopo kati ya Sh. milioni 25 na 120.

Wateja hao ni wa maeneo ya Kunduchi, Mbweni, Ukonga, Manzese, Temeke, Mivumoni, Buza, Mbagala, Kiwalani na Segerea.

Magari yatakayouzwa aina ya Scania, Suzuki Escudo, Toyota Noah, Mitsubish Rosa na nyumba zilizoko maeneo ya Mtoni Kijichi, Goba, Buyuni, Kitunda, Mbagala, Yombo na Charambe.

Tangazo la Mei 23, kampuni ya udalali ya Mangwembe 2011 ilitangaza kuuza kwa mnada nyumba ya aliyekuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Burian, ambaye alikuwa mkopoji wa benki ya Exim.

Katika tangazo hilo walieleza kuwa mnada wa nyumba hiyo iwapo mkopaji atashindwa kulipa, mnada ungefanika leo.

Siku hiyo hiyo, Benki ya Akiba Commercial ilitangaza kuuza kwa mnada wa hadhara nyumba 20 na magari sita yaliyoko mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, baada ya wateja wao kushindwa kulipa mkopo.

Tangazo hilo lilitoa msharti mnada ni mshindi kulipa asilimia 25 papo kwa papo baada ya nyundo ya dalali na kiasi kilichobaki kitatakiwa kulipwa ndani ya siku 14 baada ya mnada.

Aidha, lilifafanua kuwa atakayeshindwa kulipa, asilimia 25 ya awali haitarejeshwa na mali husika itauzwa tena huku ikiambatana na masharti mengine ikiwamo ya mali kuuzwa jinsi ilivyo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here