SHARE

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameibana Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kuitaka kutoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), sababu ya kutoa gawio dogo kwa serikali ikilinganishwa na benki zingine.

Hatua hiyo ya Ndugai imekuja baada ya kuelezwa kuwa NBC ilitoa gawio kwa serikali kwa mwaka 2016/17 la Sh. bilioni 1.2.

Akifungua semina ya kwa wajumbe wa PIC na baadhi ya wajumbe wa kamati zingine zikiwamo za bajeti na sheria ndogo iliyoandaliwa na uongozi wa NBC, Ndugai alisema serikali ina hisa asilimia 30 katika benki hiyo lakini gawio linalotolewa ni kidogo na inatia shaka.

Kutokana na gawio hilo kiduchu, alisema benki hiyo inapaswa kutoa maelezo ya kina kwa PIC kwa kuwa hisa ilizo nazo za serikali hazitofautiani na zilizopo benki ya NMB.

“Haiwezekani wenzenu wamekuwa wakitoa gawio kubwa kuliko ninyi. Hapa mnakazi kubwa ya kuishawishi kamati ili kukubaliana na majibu yenu juu ya kiasi hicho cha gawio,” alisema Ndugai.

Pia alisema benki hiyo inaonyesha haina urafiki na wananchi kutokana na kutokuwa karibu nao kwa kuwa haijafungua matawi wala kutoa mikopo kama benki za NMB na CRDB zinavyofanya.

“Mkalitafakari hili na kulifanyia kazi, muwe rafiki wa karibu na wananchi kama wanavyofanya wenzao. PIC imepewa jukumu la kuangalia mashirika yote na kuona utendaji kazi wao na yako takribani mashirika 272 ambayo ni muhimu sana,” alisema.

Spika alisema hatua hiyo itasaidia serikali kujua nini kinaendelea kabla ya kuingia mikataba na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwepo.

Awali, Mwenyekiti wa PIC, Dk. Raphael Chegeni, alisema kamati hiyo inatambua serikali inavyohangaika kupata mapato kupitia kodi na mapato mengineyo.

Alisema moja ya njia za msingi za kuhakikisha serikali inapata mapato ni kufanya kazi kwa karibu na taasisi ambazo uwekezaji wake ni mdogo kama NBC. Aliitaka benki hiyo kuacha kulala na ihakikishe inafanya kazi kwa ufanisi.

“Kwa mujibu wa taarifa za benki hii kwa mwaka 2008/9 ililipa Sh. Bilioni 3.9, mwaka 2009/10 Sh. Bilioni nne, haikutoa gawio mpaka 2016/17 ambapo imetoa Sh. bilioni 1.2,” alisema.

Alifafanua kuwa serikali ina uwekezaji wa aina mbili katika taasisi mbalimbali, mkubwa na mdogo, uwekezaji mkubwa unakaguliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali wakati uwekezaji mdogo msimamizi na mfuatiliaji ni Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Dk.Chegeni alisema lengo la semina hiyo ni kufuatilia utendaji wa kazi wa taasisi hizo kuhakikisha zinakuwa na tija kwa serikali na kuchangia kwa kiwango ambacho serikali itaridhika.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema watapata nafasi ya kuzungumza na kamati kuwaelezea juu ya mwenendo wa benki.

Sabi alisema hivi sasa wanaendelea kukuza benki, na mwaka 2000 benki ilikuwa na jumla ya mtaji Sh.Bilioni 326 na hadi sasa mtaji wa benki upo wa Sh. trilion moja.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here