SHARE

SERIKALI kupitia Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, imewatahadharisha wananchi kutotumia fedha zao za akiba maalumu kwa ajili ya malengo au mahitaji muhimu kucheza michezo ya kubahatisha.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Sadick Elimsu, kutoka Bodi hiyo kupitia tangazo linalowaeleza wananchi kuwa wasiwe na matarajio makubwa wanapocheza mchezo huo.

Elimsu aliwataka wananchi washiriki michezo hiyo kwa nia ya kufurahia mchezo kwa kujiwekea kiwango cha fedha watakazotumia kwa kila mchezo na kamwe wasiende juu ya kiwango hicho.

“Hakikisha una miaka 18 au zaidi ya hiyo kabla ya kushiriki katika michezo hii mzingatie masharti ya kila mchezo na msishiriki michezo ya kubahatisha kabla hujaielewa vyema,” alisema.

Hivi karibuni, Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga, alisema bungeni kuwa nchi ilikuwa ya wakulima na wafanyakazi na wafanyabiashara, lakini sasa imeongezeka na kuwa na wacheza kamari.

“Sasa hivi wanafunzi wote wa vyuo vikuu wakipata mikopo wanajazana kwenye vituo vya kucheza kamari, wazee wakipata pensheni wanakwenda kucheza kamari, wake zetu zamani wakati unaoa unaambiwa ili uwe na maisha mazuri ukipata fedha kidogo mpelekee mke wako, ukimpelekea mke ukija kuchunguza simu yake unakuta ujumbe mfupi wa Biko, Tatu Mzuka,” alisema Mlinga.

Pia alilitaja kundi lingine la vijana ambao ni madereva wa bodaboda kwamba nao wanacheza michezo hiyo na kuishauri Bodi ya Michezo ya kubahatisha itafute namna ya kuratibu suala hilo.

Mbunge huyo alisema madhara ya kamari ni makubwa kuliko biashara nyingine.

“Rafiki yangu Msukuma alizungumzia bangi kama zao linaloweza kutuletea uchumi tukasema linamadhara, lakini mheshimiwa Spika nakwambia kamari madhara yake ni makubwa kuliko bangi, tutafute utaratibu wa kuendesha kamari isiwe kama inavyokwenda sasa,” alisema.

Mlinga alisema madhara ya kamari yanavunja nguvu kazi ya taifa ambayo zamani vijijini vijana walikuwa wakicheza mchezo wa ‘pool table’, lakini sasa wamejikita kwenye kubahatisha.

“Nguvu kazi ya vijana imepotea kwasababu vijana wanaamini watakuwa matajiri kwa matangazo yaliyoachiwa kiholela yanayowafanya vijana kuwa na tamaa kuwa nitapata kesho,” alisema na kuongeza.

“Wengine imekuwa kama ugonjwa wao, mtu yeyote anayecheza kamari hawezi kuacha na hawa walivyo wataalam wanakupa 5,000 leo umeshinda, ukishinda 5,000 huwezi kuacha hata ushinde milioni 20 hutaacha hivyo inasababisha uteja, sasa hivi watu wanakwenda kukopa kwenye vikoba ili wacheze kamari hivyo inasababisha watu kuwa na madeni kila ukienda kwenye vikoba hailipiki,” alisema.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here