SHARE

SERIKALI imesema endapo wapo watu wenye shaka kwamba wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri walioteuliwa na Rais John Magufuli, hawapo huru na hivyo wanaweza kuharibu mwenendo wa uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu waende mahakamani kuomba ufafanuzi wa kisheria.

Mwito huo ulitolewa bungeni  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika wakati akijibu swali la msingi na la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema).

Pamoja na mambo mengine, katika maswali yake, Mollel alisema upo ushahidi kuwa wakurugenzi walioteuliwa mara baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani ni wanachama wa CCM walioshindwa kwenye kura za maoni za chama hicho na kuhoji endapo ushahidi ukiwasilishwa bungeni, serikali itakuwa tayari kuwaondoa.

Akijibu hilo, Mkuchika pamoja na kuwapa mwito wa kuwataka kwenda mahakamani kufungua kesi ili kupata ufafanuzi wa kisheria, alisema wakurugenzi watendaji (DED) hao si wanaCCM kwa vile uanachama wao kwa CCM ulikoma mara tu baada ya uteuzi.

Alisema kama ilivyo desturi duniani kote, Rais au kiongozi anapoingia madarakani hupanga safu yake ya viongozi kwa namna anavyoona yeye kuwa inafaa na ndivyo alivyofanya Rais Magufuli aliyewateua wakuu wa mikoa na wakurugenzi ili wamwakilishe katika maeneo mbalimbali kwa namna alivyoona inafaa.

“Huo ni utaratibu wa kawaida na ndiyo maana baada ya uteuzi aliyeteuliwa hutakiwa kuridhia au kukataa uteuzi kwa masharti ya kuachana na siasa na kuingia kwenye utendaji wa serikali, hawa waliridhia na sisi serikalini tunawaona wanafanya kazi nzuri tu,” alisema Mkuchika.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF) aliyehoji endapo serikali ipo tayari kubadili sheria ili wakurugenzi hao wanaotiliwa shaka wasiwe wasimamizi wa uchaguzi, Mkuchika alisema kama sheria itafikishwa bungeni na kubadilishwa serikali haitakuwa na pingamizi.

“Kwa sheria za sasa hawa ndio wasimamizi wa uchaguzi. Kama wabunge wataona sheria hii haifai basi wanaweza kujenga hoja ili sheria hii iletwe hapa bungeni na tuibadilishe,” alisema Mkuchika.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here