SHARE

WATANZANIA 112 wa kijiji cha Jasini, kata ya Mayomboni wilayani Mkinga wanadaiwa kukamatwa na kusafirishwa nchini Kenya na askari wa kikosi cha majini wa nchi hiyo wakidaiwa kuvua katika eneo la nchi hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ndiye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Maki Yona, amesema ni siku ya saba sasa Watanzania hao wameshikiliwa katika eneo la Shimoni, lakini jitihada za kuwatoa ili kuwarejea nyumbani zinaendelea.

”Mara baada ya kuwakamata nimewasiliana na balozi mdogo aliyepo Mombasa, lakini baada ya kuona muda umekuwa mdogo nikaona niwasiliane na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa ambaye ni Mkuu wa mkoa naye aweze kuwasiliana na viongozi wa ngazi ya taifa kwa ajili ya kushughulikia suala hilo,” alisema Yona.

Alisema vyombo vya sheria vya Kenya vinaendelea kufuata sheria na taratibu kwa sababu suala hilo lipo kwenye mlololongo wa viongozi wa kitaifa wa nchi hizo mbili.

Gazeti la Nipashe lilipomtafuta diwani wa kata ya Mayomboni, Hassan Ally, kujua maeneo ya mipaka katika kata yake sehemu za baharini, alisema wamekuwa wakivua katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20 na hawajawahi kuulizwa na askari wa Kenya kuwa hilo eneo ni kwao.

”Wavuvi wetu wanavua hapa Jasini takribani mwaka wa 20 na zaidi na hakuna hata siku moja walikuja na kutuuliza, lakini tunashangaa juzi walikuja na kutuambia hilo eneo ni la kwao waliporejea wakachukua hatua na kuwaweka chini ya ulinzi wavuvi wetu kisha kuwasafirsha hadi Shimoni,” alisema diwani Hassan.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, jitihada za kuwatoa na kuwarudisha nchini zinaendelea na jana jioni hatua za awali zilianza kuzaa matunda.

Nipashe ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, alisema hawajapata taarifa rasmi za tukio hilo na kumwahidi mwandishi kuwa wanaendelea kufuatilia.

”’Tunashughulikia suala hilo na hivi sasa tupo kwenye jitihada za kuwatoa kwa sababu sisi tunakaa na Wakenya kabila la Waduruma na wanafanya kazi huku na wanazaliana huku, iweje sisi tukifanya shughuli zetu katika maeneo anayodai kua ni ya kwao wanachukua hatua kali za kisheria ni vyema serikali ikaharakisha zoezi la upimaji wa mipaka ya nchi kavu na majini ili kuondoa tofauti ya nchi hizi mbili,” alisema Yona.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here