SHARE

Sakata la Amina Rafael kujifungua nje ya kituo cha Polisi cha Mang’ula Morogoro limeibuliwa bungeni leo Jumatatu Juni 11, 2018 na mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali akidai taarifa za tukio hilo zilizotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro zinaficha ukweli.

Akitumia kanuni ya 68(7) ya Bunge, Lijualikali aliomba mwongozo wa Spika, akibainisha kuwa Amina alikamatwa na polisi Juni 6, 2018 akiwa mjamzito.

“Juni 8, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani (Hamad Masauni) alilaani tukio hili hapa bungeni na alikiri huyu mama kujifungua nje ya kituo, siku hiyohiyo ofisi ya RPC Morogoro ilitoa kauli kwamba Amina hakujifungulia Polisi,” amesema Lijualikali.

“Kwa kuzingatia waziri alisema wanafanya uchunguzi ila RPC amekana nina mashaka na hili. Ninaomba ikiwezekana Amina aitwe katika Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje (ya Bunge) ahojiwe ili tupate ukweli na tukiacha taarifa hizi za RPC zitaharibu uchunguzi.”

Mara baada ya Lijualikali kumaliza kutoa mwongozo, Spika Job Ndugai amesema jambo hilo limewahi kuulizwa na mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari na Masauni alilitoa ufafanuzi, kutaka jambo hilo kupewa muda zaidi kwa kuwa hata Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa bungeni, amelisikia.

“Itafika siku tutapenda kujua majibu ya upepelezi huo. Hakuna anayetaka kujenga misingi ya polisi wetu kufanya ukatili kwa wajawazito. Tuvute muda tu. Ni jambo la simanzi, wafanye kazi na askari wana taratibu zao na wanachunguza kwa namna yao ya kushughulika,” amesema.

“Kamati ya mambo ya nje ya mwenyekiti Zungu (Mussa Azzan) huko mbele, mkija mtupatie taarifa what happen (nini kilitokea).”


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here