SHARE

Kila mtu ana namna yake ya kuonyesha furaha. Wapo wanaopiga kelele, wengine huimba na hata kucheza; lakini kwa Rashid Mashawishi ni zaidi ya hayo.

Rashid juzi alijikuta akipata Sh200,000 kutoka kwa Rais John Magufuli kwa ajili ya kuongezea mtaji wa biashara yake ya genge.

Rais Magufuli aliyekuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) unaojengwa Kinondoni, alimpa fedha hizo Rashid baada ya kufurahishwa na swali lake alilosema lilikuwa na masilahi kwa wananchi wa eneo hilo.

Katika swali lake kwa Rais, mkazi huyo wa Kinondoni alisema, “Mheshimiwa Rais hapo karibu na msikiti kuna dimbwi la maji ambalo linatufanya wakati mwingine tuwe katika wakati mgumu tunapokwenda msikitini. Kwa vile wakati fulani wewe ulikuwa mkazi wa eneo hili la Kinondoni na mimi ni mjumbe wa nyumba kumi naomba tufanyie mipango ili angalau nasi tuondokane na adha hii.”

Katika majibu yake, Rais Magufuli alisema, “Swali zuri, nadhani ameuliza kwa niaba ya wananchi napenda wananchi wa namna hii… hebu tumpigie makofi Rashid. Mkuu wa mkoa chukua namba yake ili barabara hii ianze kukarabatiwa mara moja na kazi hii ifanyike kwa fedha za mfuko wa barabara. Naagiza kazi ifanyike mara moja.”

Wakati mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akibadilishana namba na Rashid, Rais Magufuli alimuita na kumuuliza mwananchi huyo anajishughulisha na kazi gani na alipopatiwa jibu alimkabidhi fedha hizo.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi jana, Rashid alisema sehemu ya fedha hizo alinunua kuku ili kufurahia pamoja na familia yake.

Alisema kwa takriban miezi mitano hakuwahi kula kitoweo hicho, hivyo aliona ni vyema kununua kuku ili afurahi na familia yake.

“Kwa kweli nilifurahi sana na kuonyesha kwamba furaha yangu ilikuwa kubwa sikutaka jana (juzi) ipite, nilivyotoka kule (kwenye msikiti unaojengwa) nilipitiliza kununua kuku wa kienyeji wa 15,000 nile na familia yangu wakati wa daku,” alisema Rashid.

Alisema Sh70,000 alizitumia kulipa deni alilokopa kwa ajili ya ada ya mwanaye anayesoma chuo kikuu. Pia, alitumia Sh18,000 kununua nguo za sikukuu kwa ajili ya wanawe watatu. “Nimenunua kanzu mbili kila moja Sh5,000 na gauni moja la Sh8,000. Nimebakiwa na Sh87,000 mkononi ndiyo nafikiria niongeze vitu gani kwenye genge,” alisema.

Alisema baadhi ya majirani zake wanataka awapatie chochote kutoka sehemu ya fedha hizo.

‘Mgawo’ aliompa Makonda

Akizungumzia tukio la kumpatia Makonda Sh10,000 Rashid alisema, “mkuu aliniambia kwa utani na mimi utanikatia kidogo, ndiyo sababu nikampa ile hela ila baadaye alinirudishia kwa kunitumia kwenye simu.”

Rashid alisema hakuwahi kuwa na uhusiano wa karibu na Makonda, lakini anamfahamu kwa kuwa si mara ya kwanza kwake kwenda Bakwata.

Pia, alieleza iwapo barabara aliyoizungumzia itapewa jina lake kama alivyogusia Rais katika kauli yake itakuwa heshima kubwa kwake. “Nimepata faraja, naona wazi jina langu litaendelea kuwapo hata kama nikifa basi wajukuu na vitukuu vyangu watalikuta jina langu,” alisema Rashid.

Alisema barabara hiyo imekuwa ikileta usumbufu na hasa nyakati za mvua hivyo ikijengwa italeta matumaini mapya kwa wakazi wa Kinondoni Shamba.

Tangu aliposimama na kuzungumza mbele ya Rais Magufuli, Rashid amezidi kuwa maarufu mtaani kwake ambako anajulikana kwa jina la utani la Msauzi. Baadhi ya watu anaopishana nao wamekuwa wakimtania kwa kumwambia “tugawane sasa”.

Hofu ya wananchi

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa mtaa huo wana hofu iwapo ujenzi huo utaathiri nyumba zao kwa kubomolewa.

Said Makarani alisema, “tunafurahia barabara, ila lazima kuna watu watalia ndio maana unaona mtaa uko kimya kidogo, familia zimeanza kutafakari.”

Katika mtaa huo jana walikuwapo wataalamu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) wakichimba na kuchukua vipimo.

Meneja wa Tarura Manispaa ya Kinondoni, Leopold Runji alisema iwapo wataona kuna ulazima baadhi ya nyumba zitabomolewa.

Alisema historia ya eneo hilo inaonyesha halikupimwa, bali ulifanyika uboreshaji wa kutengwa maeneo ya huduma za kijamii ikiwamo barabara. “Tathmini ilifanyika na watu wakapewa maeneo huko Tegeta, ila wapo ambao hawakuondoka na wengine wakawauzia watu nyumba zao,” alisema Runji.

Alisema kinachofanyika sasa ni kupitia mchoro wa mwisho kuangalia kama wanaweza kuijenga ikiwa vivyo hivyo au barabara ipanuliwe.

Runji alisema wataalamu wa Tarura wanachukua vipimo na sampuli za udongo kwa ajili ya upembuzi yakinifu ambao hautazidi mwezi mmoja na uchunguzi ukikamilika ujenzi unatarajiwa kuchukua miezi kati ya mitano na sita.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here