SHARE

Vyama vya CCM na Chadema, leo vitapimana ubavu katika uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Monduli jijini Arusha katika mikutano miwili tofauti ya kampeni.

Kampeni za ubunge wa jimbo hilo ambalo lilikuwa CCM tangu uhuru, hadi mwaka 2015 lilipochukuliwa na Chadema zinatarajiwa kuwa za aina yake.

Julai 30, aliyekuwa mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga alijiuzulu na kujiunga na CCM na chama hicho tawala kikampitisha kuwania tena ubunge wa jimbo hilo na sasa atachuana na Yonas Laiser wa Chadema.

Uchaguzi wa majimbo ya Monduli na Ukonga na kata 23 utafanyika Septemba 16. Katika uzinduzi wa leo, Chadema watakuwa katika mji wa Mto wa Mbu, na kampeni zao zitazinduliwa na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya kampeni za Chadema katika jimbo hilo akiwa na wabunge na viongozi wengine wa chama hicho.

Lowassa alikuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 20 kupitia CCM kuanzia mwaka 1995 hadi 2015 na baadaye mwaka 2015 alijiunga na Chadema na kugombea urais, akiungwa mkono na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Upande wa CCM, kampeni zitazinduliwa na makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, Monduli mjini.

Meneja kampeni za ubunge wa jimbo hilo ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi alisema wanalitaka jeshi la polisi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki katika uchaguzi huo na kamwe hawatakubali kunyanyaswa.

Alisema kutokana na hali ya kisiasa ilivyo kwa sasa nchini, Chadema haitavumilia kunyanyaswa katika Jimbo la Monduli ambalo wanaamini ni ngome yao na mgombea wa chama hicho, Yonas Laiser atashinda.

“Tunataka tume ya uchaguzi ijue wadau wakubwa wa uchaguzi ni vyama vya siasa na hivyo, wanapaswa kushirikishwa katika kila jambo. Tumejiandaa na hatutakubali kuona jambo lolote linafanywa la ukiukwaji wa sheria,” alisema

Laiser aliomba wananchi wamchague, kwani ana ajenda ya kutatua tatizo la maji na migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.

“Tayari nimefanya kampeni za nyumba kwa nyumba kwa baadhi ya maeneo na wananchi wengi wamenielewa na nina uhakika wa ushindi,” alisema Laiser ambaye pia ni Diwani wa Lepurko

Wakati Chadema ikieleza hayo, CCM wamesema maandalizi ya uzinduzi wa kampeni yamekamilika.

Katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema jana kwamba Mangula atazindua kampeni, akishirikiana na viongozi wengine wa CCM wakiwemo baadhi ya wabunge.

“Tutazindua kampeni Monduli kesho (leo) na maandalizi yote muhimu yamekamilika na kikubwa tunakwenda kurejesha jimbo CCM kama ambavyo tumefanya katika udiwani kuzirejesha kata zote 20 zilizokuwa upinzani,” alisema Mdoe

Mdoe aliwataka wana-CCM kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni hiyo, ili kusikilizwa jinsi Serikali ya CCM inavyotekeleza ilani na mambo ambayo Wanamonduli watafanyiwa.

Katika uchaguzi huo, wagombea wengine katika jimbo hilo ni Omar Kawanga (DP), Feruzi Juma (NRA), Simon Ngilisho (Demokrasia Makini), Francis Ringo (ADA-Tadea) Elizabeth Salewa(AAFP) na Wilfred Mlay (ACT-Wazalendo).

Kampeni zaendelea Ukonga

Katika Jimbo la Ukonga, kampeni za mgombea ubunge kupitia Chadema, Asia Msangi ziliendelea jana katika kata ya Viwewe huku za mpinzani wake, Mwita Waitara wa CCM zikitarajiwa kuanza Septemba Mosi .

Akiomba kura kwa wakazi wa Viwewe na viunga vyake, Msangi alisema, “Najua changamoto kubwa katika maeneo yenu ni barabara hivyo nawaahidi kuwa nitakwenda kuwatengenezea barabara ili wananchi wapate unafuu wa kutoka eneo moja kwenda nyingine.”

Aliahidi kujenga hospitali ili wananchi wa Majohe wapate huduma za afya karibu. “Vijana nawaahidi nitafanya kazi nanyi hasa katika michezo na uchumi, najua mnapenda michezo, lakini nataka mpende pia uchumi, hivyo nakwenda kutoa elimu ya uchumi kwenu ili baada ya kujishughulisha na uchumi mchana kutwa jioni mnakwenda kwenye michezo,” alisema Msangi.

Alisema akichaguliwa atapokea ushauri kwa wazee, “Wanapoona nakosea waniite wasisite kuniambia kuwa Asia unakosea, kwa hiyo hicho ni kipaumbele changu baada ya kutangazwa mbunge.”

Kuhusu mfuko wa jimbo aliwaahidi atakuwa makini nao ili pesa ziwafikie walengwa.

“Kingine niseme, Asia Msangi nimejiandaa kuwa mbunge na najiandaa kutangazwa mbunge, Wanaukonga msiogope tunakwenda kushinda,” alisema


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here