SHARE

WAKATI Simba ikiendelea kufurahia makali ya mshambuliaji wake, Meddie Kagere, kikosi hicho kimeongezewa makali zaidi baada ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa) kumruhusu kiungo Mzambia Cletus Chama kuichezea timu hiyo, huku suala lake la Uhamisho wa Kimataifa (ITC) likiendelea kujadiliwa.

Kuruhusiwa kwa Chama ambaye hajaichezea Simba kwenye Ligi Kuu kutokana na kukwama kwa ITC , sasa kutakamilisha chama la kikosi cha Wekundu wa Msimbazi hao, ambacho kipo chini ya Mbelgiji Patrick Aussems.

Kuchelewa kwa ITC hiyo, hadi kufikia Fifa kuingilia kati na kumruhusu kuendelea kuichezea Simba suala hilo likishughulikiwa, kumetokana na klabu yake ya zamani ya Dynamos ya Zambia kugoma kuiachia kwa madai mpaka walipwe fedha zao kufuatia makubaliano waliyokuwa nayo na mchezaji huyo.

FIFA imeliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwataka wairuhusu Simba wamtumie Chama na kuwataka Dynamos kufungua kesi juu ya madai yao kwa mchezaji huyo.

Alipoulizwa Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, alisema anachofahamu ITC ya mchezaji huyo pamoja na golikipa Deogratius Munishi ‘Dida’ ziliwasili jana.

“ITC zote ya Chama na ya Dida zimefika jana, na Simba tayari imepewa taarifa,” alisema Ndimbo.

Kwa upande wake akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa Simba, Haji Manara alithibitisha kuwa Fifa wameiruhusu Simba kumtumia kiungo huyo kwenye mechi zake.

“Tunashukuru jambo hili limepatiwa ufumbuzi, Chama ataungana na wenzake kwa ajili ya kambi itakayoanza kesho,” alisema Manara.

Alisema kuruhusiwa kwa kiungo huyo kutaongeza nguvu kwenye kikosi cha kocha Aussems.

Kagere awakejeli wanaombeza

Katika hatua nyingine, baada ya juzi kufunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbeya City, straika Kagere, amesema anaamini wale wote waliokuwa wakimbeza kwa kumtaja kama mchezaji mzee wameanza kukaa kimya.

Akizungumza na Nipashe, Kagere, alisema pamoja na kuwa lengo lake kubwa ni kuisaidia timu kupata ushindi, lakini kila anapofunga anawanyamazisha wale wanaomkejeli.

“Mabao haya niliyofunga nayatoa kwao… nimekuja Simba kufanya kazi na wao waliona uwezo wangu, ninachokifanya hapa ndicho nilichokuwa nakifanya Gor Mahia, nafurahi kufunga na kuisaidia timu yangu kupata ushindi,” alisema Kagere.

Mabao mawili aliyoyafunga juzi yanamfanya Kagere kukaa kileleni mwa wafungaji bora akiwa na mabao matatu kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu baada ya awali kufunga bao pekee kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here