SHARE

BAADA ya kutokea sintofahamu na kusababisha Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Emmanuel Amunike, kuwatema wachezaji sita wa Simba, Mnigeria huyo amewasamehe nyota hao na kuahidi atawaita tena kwenye kikosi chake endapo wataendelea kuonyesha kiwango cha juu ndani ya klabu yao.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika kikao cha pamoja na kumaliza mvutano uliokuwapo kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), viongozi wa Simba na wachezaji hao ambao walitemwa baada ya kuchelewa kuripoti kambini ili kujiandaa na mechi dhidi ya Uganda.

Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, alisema kuwa TFF imezungumza na Simba na kuamua kuweka kando mvutano wa wachezaji hao na pia kocha Amunike amekubali suala hilo kumalizika na yupo tayari kuwaita wachezaji hao kwenye kikosi chake katika siku za usoni.

“Kwa sasa hawezi kuwarejesha tena kikosini kwa sababu tayari alishaita wachezaji wengine kuziba nafasi zao, na tayari wamesharipoti, ila amekubali kuwaita tena wachezaji wa Simba kwa siku za usoni kama wataonyesha kiwango kikubwa kilichomfanya awaite,” alisema Ndimbo.

Aliongeza kuwa, suala na viongozi wa Simba ambao wameitwa katika Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo kwa kosa la kusababisha wachezaji wao kuchelewa hilo lipo kwenye ofisi ya sekretarieti ya shirikisho hilo.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema linapokuja suala la kitaifa wanaweka mbele maslahi ya klabu pembeni.

“Kwa pamoja tunaungana na TFF kuisapoti timu ya Taifa, na suala la kuchelewa kwa wachezaji wa Simba kwenye kambi ya Taifa Stars tumelifunga baada ya kufikia maridhiano, tunaposhinda ni Tanzania, na tunapofungwa ni Tanzania.

” Bila kuangalia nani alikuwa na makosa, Simba tumeridhiana na TFF juu ya hili, tunaisapoti timu ya Taifa na Wanasimba wote popote walipo waisapoti Taifa Stars kwenye mchezo wetu dhidi ya Uganda, mimi na viongozi wa Simba tutaenda Uganda kuishangilia timu yetu,” alisema Manara.

Wachezaji wa Simba waliotemwa katika kikosi cha Stars ni pamoja na nahodha msaidizi, John Bocco, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here