SHARE

Wakati Yanga ikipongezwa kwa ubunifu wa kukusanya michango kutoka kwa wanachama na mashabiki, uongozi umetakiwa kutobweteka kwa mafanikio hayo.

Hadi kufikia jana, Yanga ilikuwa imevuna Sh29 milioni zilizotokana na michango ya mashabiki zitakazotumika kwa shughuli mbalimbali za uendeshaji wa klabu hiyo kongwe nchini.

Baadhi ya wadau wa michezo, wamesifu jitihada za uongozi wa Yanga, lakini wameutaka uongozi kutoa elimu kwa wanachama na mashabiki wanaotoa fedha hizo.

Pia Yanga imetakiwa kuweka bayana mapato, matumizi na ukomo wa michango hiyo kwa kuwa ni fedha zinazotolewa na watu wenye mapenzi mema na klabu hiyo.

Kitendo cha Yanga kuanzisha mchakato wa kuchangia maendeleo ya klabu hiyo kinaweza kuwa mkombozi kwa klabu hiyo katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara imekosa mdhamini mkuu. Idadi kubwa ya klabu zimeanza kuugulia maumivu kwa kukosa fedha za kuzihudumia timu zao wakati mashindano hayo yakiwa yamefikia raundi ya pili na tatu.

Waarabu waibeba Yanga

Awali, utaratibu wa kuchangia Yanga ulioanza Agosti Mosi ulikuwa wa kusuasua kabla ya fedha hizo kuanza kumiminika baada ya kuilaza USM Algier ya Algeria katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-1, katika mchezo uliochezwa Agosti 19 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Herieter Makambo na Deus Kaseke dhidi ya USM Algier, yalitosha kuwaibua mashabiki wa klabu hiyo kuchangia kwa wingi maendeleo ya klabu hiyo.

Wiki hiyo ilikuwa ya neema kwa Yanga kwa kuwa baada ya kuilaza USM Algier, ilianza vyema mashindano ya Ligi Kuu iliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Agosti 23.

Matokeo mazuri yaliyopatikana katika mechi hizo yalichochea hamasa kwa mashabiki hao kujitokeza kuchangia ambapo siku ya mchezo zilipatikana Sh2.4 milioni.

Rekodi inaonyesha siku iliyofuata Yanga ilipata Sh4.7 milioni, Agosti 25 Sh2.3, Agosti 26 Sh3.2 milioni, Agosti 27 Sh3.8 milioni, Agosti 28 Sh4.3, Agosti 29 Sh1.2 milioni, Agosti 30 Sh1.3 milioni na Agosti 31 zilipatikana Sh480,807.

Pamoja na mafanikio hayo Yanga iliwahi kukwaa kisiki baada ya kupata fedha kiduchu Sh3,907 Agosti 14. Pia Agosti 2 ilipata Sh10,253 ikiwa ni muda mfupi baada ya kupata matokeo mabaya kwa kuchapwa mabao 3-2 na Gor Mahia ya Kenya Julai 30.

Wadau walonga

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema uongozi wa klabu hiyo unastahili pongezi kwa uamuzi huo na alishauri uchangiaji huo uwe endelevu. “Inabidi wanachama wapata elimu ya kujua mchakato huo utakuwa wa muda mfupi au mrefu, lakini viongozi wana wajibu wa kutafuta namna nyingine bora ya kupata fedha ili klabu ijiendeshe yenyewe,” alisema Chambua.

Naye mchambuzi Ally Mayay alisema wanachama na mashabiki wana wajibu wa kuichangia klabu hiyo ili kuepuka dhana ya kumtegemea mtu mmoja au kikundi cha watu wachache.

“Nashauri kuwe na mipango na malengo kwa wanaosimamia michango hiyo kwa kuwa sio kila siku watu watachanga, hivi sasa kuna mwamko wa watu kuchangia lakini itafikia muda utapungua viongozi waseme ni muda gani michango hii itahitimishwa ili wajipange,”alisema Mayay.

Kauli ya Yanga

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema fedha zinazochangwa na wanachama na mashabiki zitaisaidia klabu kuiendesha timu katika maandalizi na ushiriki wa Ligi Kuu.

“Mpaka sasa michango iliyopatikana kwa mwezi Agosti Sh29 milioni, tunashukuru wanachama na mashabiki kuichangia klabu hii, tumeona jinsi mwamko ulivyokuwa mkubwa. “Licha ya kwamba malengo yetu yalikuwa kukusanya Sh100 milioni kwa mwezi, tunaamini mwezi huu malengo yetu yatatimia na hili litakuwa zoezi endelevu na tumepanga lifanyike mwaka mzima,” alisema Ten.

Yanga inapitia kipindi kigumu tangu Yusuf Manji alipoandika barua ya kujiuzulu nafasi ya mwenyekiti, hatua iliyochangia kushindwa kushiriki kikamilifu Kombe la Shirikisho Afrika.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here