SHARE

BAADA ya timu yake kupata sare ya ugenini dhidi ya Uganda, Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars), Mnigeria Emmanuel Amunike, amesema bado safari ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Afrika inaendelea na anaamini nafasi bado ipo kwa timu yake.

Akizungumza na gazeti la Nipashe jijini hapa, Amunike alieleza kufurahishwa na namna wachezaji wake walivyocheza katika mechi hiyo baada ya kuwa nao pamoja kwa muda wa siku 10 na kuongeza kuwa pointi moja kwa Uganda si jambo dogo.

Amunike alisema bado anaendelea kukijenga kikosi hicho na kueleza kuwa Afrika ina wachezaji wenye vipaji na jukumu walilonalo makocha ni kuwaongezea ujuzi ili waweze kufikia malengo.

“Nimefurahishwa na namna ya mchezo ulivyokuwa, kitu kizuri hakuna mchezaji aliyeumia, moja ya malengo yangu yametimia, wachezaji walipambana katika mechi hii na ninampongeza kila mmoja wao, namshukuru Mungu kwa matokeo haya,” alisema Amunike ambaye amerithi mikoba ya Salum Mayanga.

Mnigeria huyo alisema kwa sasa kazi yake ni kuangalia wapi wachezaji wameimarika na mapungufu yao ili aweze kurekebisha na hatimaye kuingia wakiwa imara zaidi katika mchezo unaofuata dhidi ya Cape Verde.

“Safari bado haijaisha, tunahitaji kuendelea kupambana katika mechi zinazofuata…tumekuwa na wakati mzuri sasa, lakini tunahitaji kuwa imara zaidi siku zijazo, tunarejea nyumbani kufanyia kazi yale yanayohitaji marekebisho, Afrika ina wachezaji wanaohitaji kujengwa, wana vipaji sana,” alisema Amunike.

Naye nahodha msaidizi, Himid Mao, alisema mechi dhidi ya Uganda haikuwa rahisi, lakini wanamshukuru Mungu kwa kufanya yale waliyoelekezwa na kocha wao.

“Tumepata mafanikio, hatujapoteza mchezo, tunamshukuru Mungu tumemaliza mechi salama, sisi na wenzetu hakuna aliyeumia, tunamshukuru Mungu pia kwa kutopoteza mchezo, tunaamini tutafanya vizuri zaidi katika mechi zinazokuja,” alisema Mao.

Kiungo huyo aliongeza kuwa hali ya maji iliyotokana na mvua iliyonyesha kabla ya mechi ilichangia kuharibu mchezo huo, lakini si kigezo cha wao kupata sare hiyo.

“Mechi ya ugenini huwa na mipango yake, tumefanya kile tulichoambiwa na mwalimu, tunashukuru tulichopata sio kibaya, tunajivunia, tutakuwa imara zaidi katika mechi zijazo,” Mao aliongeza.

Stars yenye pointi mbili itashuka tena dimbani ugenini kwa kuwavaa Cape Verde Oktoba 9 na Novemba 15, mwaka huu itawafuata Lesotho kwao mechi ya mwisho ikiwa jijini Dar es Salaam dhidi ya Cranes Machi mwakan


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here