SHARE

MORALI ya hali ya juu iliyopo katika kikosi cha Simba kuelekea mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, ni moja ya mambo ambayo yanazidi kumfurahisha Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems.

Aussems juzi alikishuhudia kikosi chake kikitoa kipigo cha mabao 4-2 kwa AFC Leopards ya Kenya kwenye mchezo wa kirafiki kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu iliyopo mbele yao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aussems, alisema mchezo wa juzi wa kirafiki umemuonyesha ni kwa namna gani wachezaji wake wana morali na kiu ya kufanya vizuri.

“Mchezo ulikuwa muhimu kwetu kujiweka sawa, lakini pia nilikuwa nataka kuangalia kile ninachokifanyia kazi mazoezini kimefanya kazi kwa kiasi gani,” alisema Aussems.

“Siku tano zijazo tutakuwa na mchezo wa ligi, nashukuru wachezaji wangu wamefanyia kazi makosa madogo madogo yaliyokuwa yanatunyima ushindi wa idadi kubwa ya mabao,” aliongezea kusema.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, Simba ambao wameshacheza michezo miwili ya ligi na kushinda yote, wanatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, kuvaana na wenyeji wao Ndanda FC Jumamosi Septemba 15.

Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena kuanzia Septemba 14 baada ya kumalizika kwa kipindi cha michezo ya kimataifa kwa timu za taifa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here