SHARE

BAADA ya mchezo wao wa kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Uganda ambao walilazimisha sare, kikosi cha Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kimepanga kuingia kambini mapema kujiandaa kwa mchezo ujao dhidi ya Cape Verde.

Taifa Stars itacheza na Cape Verde Oktoba 10, mwaka huu ugenini kabla ya kurudiana nchini siku tatu baadaye.Akizungumza baada ya kuwasili nchini juzi, Kocha Msaidizi wa Stars, Hemed Moroco, alisema wanatarajia kuingia kambini mapema (Septemba 24) kujiwinda kwa ajili ya mchezo huo.

Alisema kambi hiyo inatarajiwa kuwa ya wiki mbili na kikubwa itakuwa kwa ajili ya kufanyia marekebisho baadhi ya mapungufu waliyoyaona kwenye mchezo dhidi ya Uganda.

“Tunataka kuongeza kitu kwenye kikosi chetu, kambi ya mapema ni suala muhimu kwa sababu tutacheza mchezo unaofuata ‘away’ (ugenini),” alisema Morocco.

Aidha, alisema kwa wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi wanaweza wakachelewa kuungana nao, lakini kwa wale wa ndani wataanza nao maandalizi mapema.

Stars ina pointi mbili baada ya kucheza michezo miwili na yote kutoka sare, imezidiwa kwa pointi mbili na Uganda wanaoongoza Kundi lao la L, huku Lesotho ambao walitoka nao sare kwenye mchezo wa kwanza wakilingana nao pointi, Cape Verde wenyewe wanaburuza mkia kwa kuwa na pointi moja.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here