SHARE

Wakati Freeman Mbowe ataongeza nguvu kwa Edward Lowassa kufunga kampeni Monduli, CCM wametangaza kumtumia William Lukuvi ambaye anakuwa waziri wa sita kufanya kampeni katika jimbo hilo.

Uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Jumapili ya Septemba 16, huku mchuano mkali ukiwa kwa wagombea wawili, Yonas Masiaya wa Chadema na Julius Kalanga wa CCM.

Wagombea wote ni wenyeji wa Kata ya Lepurko ambayo Masiaya ni diwani wake, Kalanga kabla ya kurejea CCM alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema.

Meneja wa kampeni za Chadema, Patrick Ole Sosopi alisema Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho atafanya mkutano wa kampeni Kaya ya Monduli Mjini.

Sosopi ambaye ni kiongozi wa vijana wa chama hicho, alisema mkutano wa mwisho wa kampeni utafanywa Jumamosi na naibu Katibu mkuu Zanzibar, Salumu Mwalimu katika Kata ya Migungani.

“Tumekamilisha kampeni za chama kwa asilimia 99 na tuna uhakika wa kushinda kwa asilimia 75,”alisema Sosopi.

Kwa upande wake mgombea wa Chadema Jimbo la Monduli Yonas Masiaya ambaye pia ni diwani wa Kata ya Lepurko amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kupuuza wanaosema hata akishinda atatangazwa mgombea wa CCM.

“Tuna uhakika kushinda jimbo ambalo tunaomba watu wajitokeze kupiga kura siku za Septemba 16 bila hofu tutalinda kura zetu hadi dakika ya mwisho,” alisema.

Kwa upande wa CCM, meneja wa kampeni wa chama hicho, William Ole Nasha alisema wana uhakika wa ushindi wa asilimia 90 na kwamba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atafunga pazia la kampeni.

Alisema Waziri Lukuvi atafanya mikutano katika Kata ya Naaralami, Lepurko na maeneo mengine yenye migogoro ya ardhi na kuipatia ufumbuzi.

“Mimi niliahidi kuleta mawaziri na wamefika 10 je hao wengine wameahidi nini. Najua hawana cha kuahidi wanaomba kura bila kueleza watawafanyia nini wananchi,” asema.

Nasha akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Monduli Juu Nyumbani kwa hayati Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine alisema ujio wa mawaziri hao umekuwa na faida kubwa kwani wamejibu hoja na kutatua kero.

“Yale maeneo yenye shida ya umeme, tayari nguzo zimeanza kusambazwa, kwenye shida ya maji, sehemu yenye shida ya huduma za afya, elimu na mambo ya mazingira ufumbuzi umepatikana,”alisema.

Aliomba wananchi wa kata hiyo kulinda historia ya hayati Sokoine aliyekuwa mkazi wa eneo hilo kwa kumchagua Julius Kalanga.

Kwa upande wake Kalanga aliwaomba wananchi kumchagua kwani amehamia chama ambacho anaweza kumfikia Rais kwa urahisi.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here