SHARE

Mgombea ubunge wa Ukonga kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Salama Masoud amesema viongozi wa Chadema akiwamo Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita wameshindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika jiji hilo.

Akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo Ukonga leo, Salama alisema alitegemea jiji la Dar es Salaam linaongozwa na Chadema lingekuwa na maendeleo lakini wananchi wake bado wapo katika umasikini.

“Unawezaje kuwa Meya wa jiji halafu Rais anatangaza kuwa ukusanyaji wa mapato umepungua? hii ni aibu,” alisema Salama

Alisema jiji hilo lingeweza kukusanya mapato mengi kupitia uongozi wa upinzani lakini wameshindwa na badala yake wameliacha jiji kwa Serikali ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye analipeleka anavyotaka.

“Unapewa fursa ya kuliongoza jiji lakini unashindwa kupigania vijana wapate vibali vya kuendesha pikipiki mjini ambavyo watavilipia lakini unamuachia Makonda anatupeleka anavyotaka,” alisema.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Buyuni Chanika, Salama alisema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo ataishawishi Serikali ijenge kiwanda cha nyama.

Alisema jimbo la Ukonga lipo pembezoni na mkoa wa Pwani unaolima matunda kwa wingi hivyo atamshauri mfanyabiashara maarufu Said Bakhresa kujenga kiwanda hicho.

“Viwanda hivi vitatoa fursa za ajira kwa vijana wengi wao wanahangaika kuzitafuta mitaani,” alisema


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here