SHARE

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa mwaka 2018 umepita kwa mbinde baada ya mvutano mkali kati ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Serikali kuhusu kifungu kinachotaka migogoro inayotokea katika miradi ya ubia kuamuliwa katika mahakama za nchini.

Juzi, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee alisema kuweka kifungu kitakacholazimisha migogoro hiyo kushughulikiwa ndani ya nchi pekee kutawafukuza wawekezaji.

Akizungumza bungeni jana wakati wa kuhitimisha hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi alisema duniani kuna mjadala kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya uwekezaji, lakini nchi zinazoendelea zina msimamo mmoja wa kutoridhishwa na mfumo uliopo. “Tulichofanya Tanzania ni hatua ya kishujaa. Ni nchi chache zilizothubutu kufanya hivyo. Hayo majukwaa ya usawa ni yapi? Kuna mtu yeyote anaweza kunitajia hayo majukwaa ya usawa,” aliuliza.

“Mheshimiwa Mdee alizitaja, je nani amezitengeneza? ni World Bank (Benki ya Dunia) na ndiye mchangiaji wa fedha kwa wawekezaji wengi.”

Dk Kilangi alisema Benki ya Dunia ambaye ni mtoa fedha mkubwa kwa wawekezaji ndio waliotengeneza mfumo wa utoaji haki na hiyo mifumo ina matatizo.

“Hili lipo wazi limeandikwa na wasomi na wataalamu mbalimbali ambao si kutoka nchi zinazoendelea pekee, bali hata kwenye nchi zilizoendelea. Hawaridhiki pia na mfumo huo unadhibitiwa na watu wachache sana,” alisema.

Alisema mfumo huo wa utoaji haki unadhibitiwa na watu wasiozidi 50 kwenye kesi zote na wamejipanga.

“Wamejipanga na wanajuana na hata ukiwa na kesi wanakuambia uchague wasuluhishi ambao wamependekezwa na mahakama,” alisema.

Alisema katika mahakama za kimataifa za usuluhishi wakati mwingine sheria haziko wazi lakini pia baadhi ya wasuluhishi wanaegemea upande mmoja.

Hata hivyo Bunge lilipokaa kama kamati ya bunge zima kupitia kifungu hadi kifungu, Mdee alisema anamshangaa mwanasheria mkuu kuifananisha Tanzania na Iran ambayo ina uchumi mkubwa.

“Sisi tumerudisha sheria kama ilivyokuwa awali…Naomba haya mabadiliko yaliyoletwa na Serikali yaondolewe ili kutoa fursa kwa migogoro kutatuliwa ndani ama nje ya nchi kwa kadri atakavyoona mwekezaji,”alisema.

Akijibu hilo, Dk Kilangi alinukuu hotuba ya kambi hiyo kuhusu muswada huo iliyosema, “mwekezaji yeyote makini anataka kwenda katika mahakama ya usuluhishi wa masuala ya kibiashara ambazo ziko neutral”

Alisema kama Serikali itakubali mapendekezo ya Mdee ni mtego ambao utawekwa na wawekezaji watatafsiri kuwa usuluhishi unaweza kufanyika ndani au nje ya nchi.

“Msimamo wa Serikali ni kwamba haya yote yafanyike ndani ya nchi,”alisema.

Hata hivyo, Mdee aliendelea kung’ang’ania hoja yake na kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumalizia sentensi katika hotuba yake.

Aungwa mkono, apigwa

Hoja ya Halima iliungwa mkono na John Heche (Tarime Vijijini-Chadema) na Ally Salehe (Malindi-CUF) ambao walitaka kuwe na fursa ya usuluhishi mahakama za ndani na nje ya nchi ili kuvutia wawekezaji wengi na makini.

Hata hivyo, Mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene alisema ni lazima kujiuliza usawa uko wapi kwa sababu kampuni zinazotumia mahakama za kimataifa ndizo zinazofadhili.

“Lakini Tanzania kama nchi ambayo tuna mfumo wa sheria,, tuna nchi huru yenye, kati yetu sisi wenyewe tunadharau mfumo wetu wenyewe kuna mashaka makubwa ya uzalendo wa baadhi ya wenzetu,”alisema.

Naye Dk Kilangi alisema mikakati mikubwa inayofanywa na wawekezaji ni kuzitisha nchi zinazoendelea.

Baada ya michango hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alisema hoja ya Serikali ni ya msingi na mara nyingi upinzani wamekuwa wakiitahadharisha kuhusu kushindwa katika kesi mbalimbali za usuluhishi.

“Cha ajabu kila tukishindwa kesi za kimataifa watu kwenye mitandao wanafurahi kabisa, tumepigwa, tumepigwa sasa leo rasilimali za nchi si mapapai. Haziozi wala hazitaoza,”alisema.

Alisema raslimali za nchini ni lazima zitumike kwa manufaa ya watu na sio kwa wawekezaji tu.

Akimalizia hoja yake, Mdee alisema wabunge wa kambi hiyo hawacheki serikali inaposhindwa kesi za kimataifa bali huwakebehi kwa sababu wanapuuzwa pindi wanapoishauri serikali.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here