SHARE

Mgombea ubunge Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara amesema amekataa kuwa kenge kwenye safari ya mamba ya Chadema.

Waitara alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Bombambili eneo la Kivule kwenye kampeni ya kuomba ridhaa ya kuongoza tena Jimbo la Ukonga.

Alisema baadhi ya viongozi wa Chadema akiwamo Freeman Mbowe, kwenye majimbo yao kuna huduma muhimu ilihali yeye kwake kuna shida ya maji, umeme, barabara ndiyo maana hawaoni shida kuwakataza wenye majimbo yenye hali mbaya kama lake kuonana na mawaziri wenye dhamana.

“Mbowe jimboni kwake Hai kuna umeme hadi migombani, Mbeya kwa Sugu kuna halikadhalika, nikitaka kuonana na mawaziri ambao nitashirikiana nao nakatazwa.

“Waswahili wanasema kwenye safari ya mamba na kenge wamo, nimekataa kuwa kenge kwenye safari ya Chadema kwa sababu mimi najua Bombambili kuna shida ya barabara, maji na umeme. Naonekana ni mbunge nisiyefanya kazi, jimbo langu lina changamoto nyingi nimejiongeza,” alisisiza Witara.

Kwa mujibu wa Waitara, amefuata mafunzo ya wahenga yasemayo akili za kuambiwa changanya na zako, hivyo ameamua kuzichanganya na kuamua kuhama.

Alifafanua kuwa amejiridhisha bila shaka kuwa kwa siku za hivi karibuni kwa uongozi wa Mbowe hadhani kama atashika dola.

Alisema kwa mchezaji wa mpira siku zote ana mawazo ya kucheza timu itakayokuwa bingwa; “kwa upinzani huu utasubiri sana, nimeamua nijiunge na timu inayocheza ligi kuu nimeachana na wale wa mchangani,” alisema Waitara.

Waitara alidai kuwa hata aliposhinda jimbo hilo ni juhudi zake binafsi na wananchi wa Ukonga na siyo Chadema.

Alisema aligombea akiwa kama yatima alikusanya michango mwenyewe, kampeni meneja mwenyewe na hakuna hata mmoja kutoka Chadema aliyemsaidia.

“Tumalizeni hili la ubunge halafu tutakuja kuzungumza la udiwani, kwani tunataka kuwang’oa wote waliobaki ili tuongee lugha moja kwa ajili ya maendeleo ya wana-Ukonga, ” alisema Waitara.

Alisema hataki kujibizana na Chadema kwa mambo wanayosema kwenye mikutano yao, lakini kama yupo anayetaka kuona vyeti vyake yupo tayari kuvionyesha hadharani na kwamba viongozi wa chama hicho wameamua kusema uongo.

Kwa upande wa mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (Kibajaji) alisema matatizo ya wananchi wa Ukonga yatapata suluhu iwapo watamchangua mbunge mwenye mawasiliano na Serikali.

Alisema hakuna kiongozi anayeweza kutatua kero za wananchi kama hana mawasiliano na viongozi wa Serikali na kwa Waitara anayo nafasi kwa sababu atakuwa anakutana nao ndani na nje ya bunge.

Alisema Waitara anapaswa kupewa kura ili atatue tatizo la jimbo hilo .

“Pimeni kazi atakazofanya Asia Msangi wa Chadema kisha angalieni kazi za Waitara. Waitara ameshafanya kazi bungeni kwa miaka miwili anajua kila kitu, tunatafuta mbunge hatutafuti watu wa kwenda kuwamfundisha choo cha bunge kilipo,” alisisitiza mbunge huyo machachari.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here